Header Ads Widget

SERIKALI YATOA BILIONI 21.7 KWA MKOA WA TABORA ILI KUBORESHA MIUNDOMINU YA SEKTA YA ELIMU NA AFYA

SERIKALI imetoa kiasi cha shilingi bilioni 21.7 kwa Mkoa wa Tabora  kupitia Mpango wa Maendeleo ya Ustawi waTaifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya elimu na afya.

Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 17 ni kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya elimu katika Shule za Sekondari na Vituo Shikizi vya Shule za Msingi.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani wakati akihutubia kikao cha robo ya kwanza cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui.

Alisema kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi bilioni 11.7 zitakwenda kujenga madarasa 585 katika Sekondari za Halmashauri zote tayari kwa ajili ya kupokea wanafunzi ambao watakuwa wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha kwanza hapo mwakani.

Balozi Dkt. Batilda alisema kiasi  kingine cha shilingi bilioni 5.3 zitatumika katika ujenzi wa madarasa 266 katika Vituo vya Shikizi vya Shule za Msingi.

Aliongeza kuwa kiasicha shilingi  milioni 160 zitatumika katika ujenzi wa mabweni kwa shule za watoto wenye mahitaji maalum.

Balozi Dkt. Batilda alisema shilingi milioni 550.9 ni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya upelekaji wa maji kwenye Shule ikiwemo ya kunawa mikono, uvunaji wa maji ya mvua , kuchimba visima katika shule 28 za Msingi na Sekondari .

“Kwa kweli Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan , sisi watu wa Tabora imetuheshimisha sana …kwa kipindi kifupi cha uongozi wa Mama Samia tumepata fedha nyingi kwa ajili ya uboreshaji wa upatikanaji wa huduma za afya , elimu, maji na barabara tunasena Wabhezya sana Mama Samia Suluhu Hassan” alisisitiza.

Balozi Dkt. Batilda alisema kufuatia heshima kubwa waliopewa amesimamisha kwa muda safari za nje ya Mkoa kwa Watumishi wa umma katika kipindi cha utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa ya Sekondari na Shule Shikizi ili yakamilike kwa wakati.

Alisema watumishi hao wanatakiwa kwenda kwenye maeneo ya miradi ya ujenzi kwa ajili ya kuhakikisha wanasimamia ili imalizike kabla ya Mwezi Desemba na kwa ubora uliokusudiwa.

Aidha Balozi Dkt. Batilda alisema Serikali haitamuonea huruma mtu yoyote atakayetumia fedha hizo kinyume cha malengo yake.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI