Alisema hayo ili makundi ya nyuki yasije yakapotea kutokana na matumizi ya viwatilifu ikiwemo salfa ambavyo vinaweza kusababisha vifo kwa nyuki wakati wanakwenda kwenye maua kutafuta chavua.
Balozi Dkt. Batilda Buriani alitoa kauli hiyo leo wakati akihutubia kikao cha robo ya kwanza cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui.
Alisema asali ni nembo ya kielelezo kikubwa cha Mkoa wa Tabora kwa hiyo shughuli yoyote ya kuathiri makundi ya nyuki si vema ikafanyika.
Balozi Dkt. Batilda aliongeza kuwa nyuki wanazofaida nyingini ikiwemo uchavushaji mimea ya mazao mbalimbali na uzalishaji wa asali na mazao mbalimbali ya nyuki.
Balozi Dkt. Batilda alisema vitendo vya kuhatarisha maisha yao vinahatarisha pia maisha ya wakazi wa Tabora kwa kupoteza utajiri wa asili wa asali na kudhoofisha uzalishaji wa mazao mashambani.
Alisema kimsingi hapingi ulimaji wa Korosho katika Mkoa huo bali kinachotakiwa kuangaliwa kwa upana ni faida na hasara zitakazopatikana kutokana na matumizi ya viwatilifu kwenye korosho dhidi ya uzalishaji wa asali.
Balozi Dkt. Batilda alisema ni vema watafiti wa wadudu na wale wa kilimo wakashirikiana ili kuja na msimamo wa aina moja katika suala la kilimo cha korosho Mkoani Tabora.
Alisema Mkoa huo uko katika mkakati mkubwa wa kutengeneza mazingira ya kisasa ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki.
Aidha Balozi Dkt. Batilda alisisitiza kuwa yapo mazao mengi ya kudumu nje ya korosho kama vile michikichi ambayo yakilimwa Mkoani humo hayana athari kwa nyuki.
0 Comments