Madereva wa bajaj na bodaboda mkoani Iringa wametakiwa kuwaheshimu askari wa usalama barabarani pindi wanapokuwa wanatumia vyombo vya moto barabarani. mwandishi wa matukio daima Diana Bisangao anaripoti kutokea Iringa
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga alipokuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya Nenda kwa Usalama yaliyofanyika leo Novemba 9 katika viwanja vya stendi ya zamani mkoani hapo, ambapo kauli mbiu ya maadhimisho ikisema ''JALI MAISHA YAKO NA YA WENGINE BARABARANI''
Sendiga alisema baadhi ya madereva wa bajaj na bodaboda wamekuwa ndio wavunjifu wakubwa wa sheria za barabarani na hivyo kuwataka wawe makini kwani atakayekamatwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa juu yake pamoja na mmiliki wa chombo hicho.
''nilipata kushuhudia tukio moja kwa macho yangu mawili trafiki anamsimamisha dereva wa bajaj, akaja kama anataka kusimama alivyofika karibu na trafiki akaongeza spidi akimuelekea trafiki alipokuwepo, kwahiyo yule trafiki ikabidi akimbie kumkwepa dereva asimgonge, nikamuita yule trafiki nikamuuliza hiki ni kitu gani akaniambia mkuu hii ni hali ya kawaida kwa mkoa huu madereva wa bajaj na bodaboda wanatudharau sana''
Sendiga aliendelea kusisitiza kuwa anahitaji askari wake waheshimiwe kwa kupewa nguvu ya kufanya maamuzi ya kuwanyoosha vijana wachache wanaoharibu na kuchafua nidhamu ya udereva pia alitoa onyo kwa wamiliki ambao wengine ni maaskari wa mkoa huu kuwafundisha nidhamu madereva wanaowapa vyombo vyao vya moto na kutii alama za usalama barabarani na hivyo wakikamatwa hata kama bajaj ni ya mkubwa mahali fulani basi sheria zitachuliwa kwa dereva pamoja na mmiliki.
''baadhi ya hao vijana wanaochafua hadhi ya barabarani wakikamatwa wakipelekwa polisi sheria iende kufanya kazi kwa sababu trafiki nao wanalalamika, wakiwakamata hao vijana inasemekana kuna baadhi ya bajaj zinamilikiwa na baadhi ya maaskari wangu , hivyo madereva wanakuwa na jeuri kupitiliza kwa askari atakayewakamata, naomba niwaambie trafiki ukimkamata dereva akakuletea kujua kwakuwa chombo anachoendesha kinamilikiwa na askari mwingine mwenye cheo kikubwa kuliko wewe usipate stress nipenyezee kataarifa ili nianze kumnyoosha mmiliki na dereva wake maana kwenye nchin hii hakuna aliye juu ya sheria, mji lazima ukae kwenye sheria na taratibu zinazostahili. alimalizia Sendiga
Pia mkuu huyo aliwasisistiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya UVIKO 19 ili kujikinga na ugonjwa huo hatari.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohammed Hassan Moyo aliwataka wananchi kuweka kipaumbele swala la kutii sheria bila kushurutishwa na kuwaomba polisi na afande kutumia mamlaka yao kutoa elimu ya matumizi ya vyombo vya usalama barabarani kwa wananchi na pia kutoa adhabu kwa madereva ambao wanavunja sheria za barabarani.
Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa ACP Juma Bwire alisema matukio ya ajali za barabarani yamepungua kwa asilimia kubwa kwa mwaka 2021 ukilinganisha na mwaka jana (2020) na kuwasisitiza wananchi kutumia barabara vizuri.
''takwimu zinaonyesha kipindi cha January mpaka Oktoba mwaka 2020 ajali zilizolipotiwa ni 28, watu waliokufa ni 48 wanaume 41 wanawake 7, watu waliojeruhiwa 68 wanaume 43 wanawake 25, na kwa January hadi Oktoba 2021 ajali zilizolipotiwa ni 24, vifo 29 wanaume 18 wanawake 11, majeruhi 36 wanaume 28 na wanawake 8 kwahiyo inaonyesha kwamba tumeweza kupunguza ajali 4, vifo 19 na majeruhi 32.'' alisema Bwire
0 Comments