Chuo cha taifa cha usafirishaji (NIT) kupitia Kituo cha umahiri cha kikanda cha usalama barabarani kimetoa mafunzo ya usalama barabarani kwa wanafunzi kutoka shule kumi 10 za mkoa wa Arusha pamoja na madereva Bodaboda ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya wiki nenda kwa usalama barabarani.......NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Akiongea na waandishi wa habari Dkt Omar Mashi mkuu wa kituo cha umahiri cha kikanda katika masuala ya usalama barabara alisema kuwa kama chuo kunawezesha wanafunzi kwa kuwapa elimu, mabango na vipeperushi lengo likiwa ni kuwafanya kutumia barabara kwa usahihi na kuepuka madhara yanawoweza kutolea pale watakapotumia barabara vibaya.
“Tumeandaa mabango na vipeperushi na kugawa katika shule mbalimbali za msingi lengo likiwa ni kuwasaidia wanafunzi katika matumizi sahihi ya barabara lakini pia tumetoa elimu katika vituo mbalimbali vya Bodaboda hapa katika jiji la Arusha na hii itasaidia kuwepo kwa matumizi sahihi ya barabara kwa watumiaji wote,”Alisema Dkt Mashi.
Alifafanua kuwa lengo hasa ni kutoa elimu juu ya sheria za barabarani lakini pia wana programu mbalimbali wanazoziendesha ikiwemo kuandaaa mitaala na kufanya utafiti katika masuala ya usalama barabarani ambapo kama tasisi ya Elimu ni lazima wawe na takwimu za kutosha juu ya usalama barabarani ambayo ni pamoja na ajali zinazotokea.
“Ajenda mojawapo tuliyonayo ni yakufanya utafiti katika masuala ya usalama barabarani na kama kitengo wanawashauri madereva wote na watu wanaotaka kutumia vyombo vya moto kuwa na ulazima wa kupata elimu sahihi na katika chuo sahihi kwani kitendo cha kupata leseni pembeni bila kufuata utaratibu ni hatari kwani ndio chanzo cha ajali nyingi na bila kupata elimu hiyo ajali zitaendelea kutolea kutokana na uzembe wa madereva,”alisema.
Kwa upande wake Pascal Duwe mkufunzi kutoka chuo hicho alisema kuwa mafunzo waliyotoa kwa madereva Bodaboda yamelenga mada za usalama wao, usalama wa chombo chao, usalama wa watumiaji wa chombo chao pamoja na usalama wa watumiaji wengine wa barabara ambapo pia yamelenga kutii Sheria na matumizi ya chombo hicho.
“Katika kutoa mafunzo haya tumejitahidi kuwafikia madereva mahali walipo na wameweza kuitokia wito ambapo tumewafunfisha mambo mengi ikiwemo mavazi wanayopaswa kuvaa wakati wanaendesha ambayo ni mavazi magumu na yanayorejesha mwanga pamoja na sifa ambazo vyombo vyao vinapaswa kuwa navyo mojawapo ikiwa ni taa na viongoza vingine,” Alisema Duwe.
Alifafanua kuwa pia wamewafundisha kuzingatia kanuni za kuendesha vyombo hivyo hasa wakati wa kupita magari yaliyo mbele kwa kuzingatia sheria na kufuata alama na michoro ya barabarani hasa maeneo ya vipambele kama vivuko vya waenda kwa miguu na kwenye makutano.
Mmoja wa wanafunzi kutoka shule ya msingi Meru Halifa Fadhili alisema kuwa wamefundishwa Sheria za kufuata wakati wa kuvuka barabara ambapo mojawapo ni kutafuta sehemu salama ya kuvukia, kusimamia kwenye ukingi wa barabara, kuangalia maagari kulia na kushoto na sehemu zote kuzunguka barabara na kusikiliza,kama kuna gari linakuja kuliacha lipite, wakati hakuna gari linalokuja vuka moja kwa moja bila kukimbia pamoja na kuangalia na kusikiliza magari wakati unavuka.
Dereva Bodaboda kutoka kata ya Ungalimited Kisali William Ayo alisema kuwa wengi wao walikuwa hawazijui sheria za barabarani hali iliyopelekea kutokea kwa ajali mara kwa mara lakini anaamini baada ya elimu hiyo watatilia maanani Sheria za barabara na kuweza kuepuka ajali zinazosababishwa na uzembe wa madereva.
“Awali ilikuwa mtu ukiwasha chombo chako unaelekeza tu uelekeo unataka kwenda lakini sasa hivi tumejifunza mambo mengi juu ya usalama wetu, abiria na watumiaji wengine wa barabara hivyo shukrani ziwaendee chuo Cha NIT kwa kuona umuhimu wa kutupa elimu,” Alisema Kisali.
Naye Mosi Boniface mkuu wa kitengo cha elimu kwa umma kutoka makao makuu ya polisi alisema kuwa wapo katika wiki ya nenda kwa usalama barabarani ambapo wanashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo NIT kutoa elimu ya usalama barabarani lengo likiwa ni kuwakumbusha watumiaji wote wa barabara matumizi sahihi ya barabara ili kuondokana na ajali zinazoweza kutokea.
0 Comments