Header Ads Widget

MIKOPO YATOLEWA KWA VIKUNDI MKOANI KILIMANJARO




 Na Rehema Abraham


Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro Juma Raibu amekabidhi mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 295,955,000 kwa vikundi 44 vya wanawake 31 ,vijana 11 na watu wenye ulemavu ili fedha hizo ziweze kuwasaidia katika kujikwamua kiuchumi.


Akizungumza  mara bàada ya  kukabidhi mfano wa hundi ya fedha za mikopo kwa vikundi hivyo , Meya huyo amevitaka vikundi hivyo kwenda kutumia vyema mikopo  waliyoipta kama ilivyo kusudiwa.



"Wiki iliyopita tumekamata akina mama na vijana kwa sababu ya kuchukua mikopo na kwenda kununua wigi na makochi jambo ambalo mwisho wa siku wanashindwa kurejesha mikopo ya halmashauri "Alisema Juma.



Katika hatua nyingine amesema fedha hizo zisizo na riba zimesaidia wananchi walio wengi ambao wamejiunga kwenye vikundi na kwamba fedha hizo ni kwa ajili ya kwenda kuchochea maendeleo.



Awali akisoma taarifa ya Mikopo hiyo Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya jamii Manispaa ya Moshi Rose Minja amesema Halmashauri imeendelea kuhamasisha Wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu kuunda vikundi vya kiuchumi kwa lengo la kujiongezea kipato pamoja na kupata fursa ya kufaidika na mikopo hiyo na Elimu ya mikopo kwa wananchi imekua ikitolewa hasa kwa vikundi vinavyoomba mikopo.


Amesema licha ya kuwepo kwa mafanikio makubwa katika utoaji mikopo hiyo zipo changamoto kwa baadhi ya vikundi kuwa wadanganyifu na kuandaa miradi hewa,watu wenye ulemavu kuwa na mwamko mdogo wa kuomba mikopo hiyo pamoja na baadhi ya vikundi kutozingatia mkataba wa kukopa na kushindwa kurejesha.


Naye Diwani wa Kata ya Majengo Hamphey  Mosha amewapongeza wajasiriamali waliopata mikopo hiyo huku akiwahimiza kutumia fedha hiyo kwa malengo na kwamba washirikiane kwenye vikundi vyao ili shughuli ziweze kufanyika kwa uwazi na ufanisi.




Kwa upande wake mmoja wa wajasiriamali hao mwenye ulemavu Aman Amede ameshukuru kwa kupata mkopo huo ambao watautumia katika kufanikisha malengo waliyojiwekea.



Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita 2015 hadi machi 2021 Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imefanikiwa kukopesha kiasi cha zaidi ya bilioni 2 kwa vikundi vya wanawake vijana na watu wenye ulemavu.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI