Header Ads Widget

MAKONDA KUMFUATA OLE SABAYA GEREZANI?

 

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Christian Makonda, anatarajiwa kufikishwa mahakamani, wakati wowote kuanzia sasa.

Makonda anatarajiwa kufikishwa mahakamani, pamoja na mambo mengine, kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka ikiwemo kuvamia kituo cha televisheni cha Clouds Media, Dar es Salaam.

‘’nakwambia hivi, mchakato wa kumfikisha Makonda mahakamani, tayari umeiva. Muda wowote wiki hii, kesi yaweza kufunguliwa nay eye kupelekewa mwito wa kutakiwa kuja kujitetea,’’ anaeleza mmoja wa mawakili ambaye amepewa jukumu la kufungua shauri hilo.

Kupatikana kwa taarifa kuwa Makonda yuko hatarini kufikishwa mahakamani, kunakuja huku Mkuu wa Wilaya ya Hai, Kilimanjaro, Lengai ole Sabaya akitumikia kifungo cha miaka 30 gerezani.

Sabaya na wenzake watatu walihukumiwa kifungo hicho na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha mwezi uliopita baada ya kupatikana na hatia ya wizi na unyang’anyi wa kutumia silaha.

Aidha, Sabaya na wenzake sita wanakabiliwa na mashtaka mengine kadhaa, ikiwamo kuendesha genge la uhalifu, uhujumu uchumi, utakasishaji fedha na matumizi mabaya ya madaraka.

Wote wawili Sabaya na Makonda waliteuliwa kushika nyadhifa zao na Rais John Magufuli ambaye alifariki dunia Machi 17 mwaka huu.

Miezi miwili baadaye, Rais Samia Suluhu Hassan aliyemrithi Magufuli akatangaza kumsimamisha kazi Sabaya ambaye aliwahi pia kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UV-CCM), Mkoa wa Arusha, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizokuwa zikimkabili.

Baadhi ya wachambuzi wa kisiasa na utawala bora, wanawataja Sabaya na Makonda kuwa mfano wa viongozi wababe waliovunja sheria na kwenda kinyume na maadili ya kazi zao lakini walikuwa hawaguswi kwa madai kwamba walilindwa na mamlaka zao za uteuzi.

Kwa mujibu wa maombi yaliyopo, Makonda anadaiwa kuvamia kituo hicho cha televisheni cha Clouds na kuingilia maudhui ya kipindi cha Shilawadu, Machi 17, 2017.

Mashtaka dhidi ya Makonda yanafunguliwa na Mwanasheria wa kujitegemea anayefanyia shughuli zake Dar es Salaam. Mwanasheria huyo ameomba kibali cha Mahakama kumshtakiMakonda kutokana na makosa anayodaiwa kuyatenda wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kinyume cha sheria namba 96.

Makonda anadaiwa kuwa siku hiyo ya Machi 17, 2017 saa 3;40 usiku katika ofisi za Clouds Mikocheni akiwa na watu wengine wanaoaminika kuwa ni walinzi wake, alivamia kituo hicho cha utangazaji

Kwamba siku hiyo Makonda na kundi lake walimfuata mtangazaji wa kipindi cha Shilawadu na kumlazimisha arushe video inayomwonesha mwanamke aliyejulikana kwa jina la Grace Athuman, ambaye anadaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kinyume cha taratibu na kanuni walizojiwekea katika kazi zao.

Video hiyo ambayo haijulikani ilirekodiwa wapi na nani, inadaiwa kumwonesha Grace akieleza kwa undani uhusiano wake na Askofu Gwajima, hali ambayo ingeweza kuchafua jina na heshima ya kiongozi huyo wa kiroho na familia yake.

Ikumbukwe kuwa wakati Makonda anavamia Clouds na kulazimisha kurushwa kipindi hicho, alikuwa na vita vya maneno na Askofu Gwajima. Kwa mujibu wa hati hiyo ya mashitaka, kosa la pili ambalo Makonda anakusudiwa kuburuzwa nalo kortini ni kuingilia maudhui ya matangazo ya Clouds kinyume na sheria.

Katika maombi hayo mlalamikaji ameambatanisha taarifa ya Kamati iliyoundwa na aliyekuwa Waziri wa Michezo, Nape Nnauye. Taarifa ya Nape iliyotaka Makonda achukuliwe hatua za kiwajibikaji na mamlaka yake ya uteuzi haikufanyiwa kazi, kwani muda mfupi baada ya kusoma sehemu ya ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari, Rais Magufuli alitengua uteuzi wake.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo ni Deodatus Balile ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa The Guardian, Jesse Kwayu na Mkurugenzi wa Upendo Radio, Neng’da Johanes. Wengine ni Mabel Masasi, wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Dk Hassan Abbas ambaye wakati huo alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari(Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali).

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, pamoja na Kamati hiyo kujitahidi kumtafuta Makonda kwa ajili ya mahojiano, kiongozi huyo alikataaa katakata kufika mbele yake.

Matokeo ya Kamati

Kamati hiyo ilithibitisha kuwa Makonda alivamia kituo cha Clouds saa nne usiku, akiwa anaendesha mwenyewe gari namba T553BFM.

Kamera za CCTV na kitabu cha kumbukumbu za walinzi kilionesha kuwa Makonda aliingia akiwa na askari wane waliokuwa na sare tofauti za majeshi ya ulinzi na usalama, kati yao watatu wakiwa na silaha za moto.

Pia kamati hiyo imethibitisha kuwa Makonda na askari wake waliingia hadi chumba cha utangazaji jambo ambalo ni kinyume na kanuni za utangazaji.



Ripoti hiyo ilibainisha kuwa katika hatua hiyo ambayo ni kinyume cha sheria, Makonda alitumia vitisho dhidi ya wafanyakazi wa Clouds kwa kutumia silaha za moto. Aidha, Kamati hiyo ilibainikuwepo uvunjaji wa sheria ya habari ya mwaka 2016 kwa kitendo cha kuingilia uhuru wa uhariri na vyombo vya habari kwa kiwango cha juu kutokana na vitisho na amri alizotoa.

Maoni ya Kamati yalibaini kuwa vitendo vya Makonda vinaashiria uvunjifu wa sheria za nchi, hususani zinazohusu utangazaji na huduma ya habari.

Kamati ilibaini dalili za Makonda kutotambua ukubwa wa madaraka aliyonayo na kujikuta anayatumia vibaya katika mazingira yasiyostahili.

Pia kamati ilibaini kuwa uongozi wa Clouds ulistahili pongezi kwa kusimamia misingi, sheria na maadili ya uandishi wa habari kwa kukataa kurusha habari isiyo na mizania.

Mapendekezo ya Kamati hiyo yalimtaka Makonda awaombe radhi wafanyakazi wa Clouds na vyombo vya habari nchini kwa tukio hilo la ukiukwaji wa usalama na maadili ya uandishi wa habari.

Aidha, kamati ilipendekeza aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati huo Nape awasilishe ripoti hiyo kwa mamlaka ya uteuzi ili ichukue hatua stahiki.

Mapendekezo mengine yalikuwa ni kuvitaka vyombo vya Dola kuanzia uchunguzi dhidi ya askari walioingia kwenye chumba cha habari na silaha za moto ili kuzuia matukio kama hayo kutokea wakati mwingine.

Kamati ilipendekeza kwa Clouds Media kupitia miongozo, kanuni na sheria zinazoongoza shughuli za utangazaji na kuangalia njia bora ya kuwa na udhibiti kwa watu wasiohusika kuzoea kuingia mara kwa mara na kufanya kazi za uhariri bila wanataaluma wa habari au wahusika katika chumba cha habari.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI