Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango jana tarehe 10, Novemba 2021 alifungua warsha ya utafiti ya REPOA ya 25 ,iliyoandaliwa kwa kushirikiano na Wizara ya Viwanda na Biashara. Warsha hiyo ya mwaka 2021 limebeba dhima ya Mageuzi ya uchumi wa Tanzania kupitia uzalishaji viwandani na biashara shindani.
Akifungua Warsha hiyo Makamu wa Rais alisema katika karne ya 21 Taifa haliwezi kupata maendeleo ya haraka pasipo kutumia tafiti kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia mara kwa mara hivyo utoaji maamuzi pamoja na kupanga mipango ya maendeleo kunahitaji kuongozwa na matokeo ya tafiti.
Makamu wa Rais alisema serikali ya awamu ya sita itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa watafiti wa ndani katika kuwawezesha kuzalisha tafiti za sera zenye ubora pamoja na kuwahusisha katika majadiliano wakati wa utungaji wa sera mbalimbali za taifa.
Alisema katika kukuza uchumi shindani serikali ya Tanzania imeendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu, ukuzaji ujuzi pamoja na elimu ya ufundi ili kuendana na mazingira shindani pamoja na ukuaji wa haraka wa teknolojia.
Aidha Makamu wa Rais aliziasa sekta binafsi kuendelea kutoa mchango wao katika kukuza uchumi shindani ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika kuwajengea uwezo vijana ili kuwawezesha kuwa na ufanisi katika kazi, aidha alitoa wito kwa wadau wa maendeleo kuendelea kutoa mchango wao katika vipaumbele vya taifa pamoja na kuwasihi watanzania kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na uwazi ili kuliletea taifa maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA Dkt. Donald Mmari alisema warsha hiyo ni muhimu kwa kuwa inatoa nafasi kwa watunga sera na viongozi kusikia matokeo ya tafiti pamoja na uzoefu wa nchi nyingine ili kuhuisha mipango na sera za Tanzania katika kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka zaidi.
Aidha alisema dhima inayotumika katika warsha hiyo inauwiano na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa unaolenga kuimarisha uchumi wa viwanda ili uwe shindani katika kupata masoko , mitaji, pamoja na rasilimali za uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya ajira na ustawi wa wananchi.
Aidha Dkt. Mmari aliongeza kwamba kutokana na kubadilika kwa teknolojia ya viwandani katika mapinduzi ya nne ya viwanda, tafiti zinaonesha nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania hazina budi kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wenye tija na ajira kwenye sekta za kati pamoja na sekta ndogo zenye uwezo wa kuwa shindani kwa muda mfupi.
Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Viwanda na Biashara Prof Kitila Mkumbo alisema serikali inatambua mchango wa taasisi za utafiti hapa nchini na itaendelea kupokea matokea ya tafiti hizo katika kuboresha utendaji serikalini.
Alisema warsha hiyo itasaidia mpango wa serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara wa kuandaa mpango maalum wa utekelezaji wa sera ya viwanda nchini huku akisisitiza sekta ya viwanda ni muhimu katika uchumi shindani utakaoweza kutoa ajira na kuondoa umasikini kwa wananchi.





0 Comments