Kijiji Cha Chemchem kilichopo kata ya Arusha Chini Halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro hakina barabara ya kuunganishiwa kijiji hicho na maeneo jirani tangu tulivyopata uhuru jambo linalowapa adha wananchi wa maeneo hayo wakati wakufuata huduma za kijaa kwenye maeneo jirani.Mwandishi wa Matukio Daima Gift Mongi anaripoti toka Kilimanjaro
Kutokana na kadhia hiyo wananchi hao hukosa mawasiliano hususan msimu wa mvua ambapo eneo hilo huwa na mafuriko na wananchi kutumia mitumbwi kuvuka kwenda wilaya ya Simanjiro kwenda kupata matibabu badala ya hospitali ya TPC iliyopo eneo la karibu.
Mwenyekiti wa hijiji hicho Alex Joseph alisema Hadi Sasa msaada uliofanywa na taasisi ya FT Kilimanjaro iliyopo chini ya TPC kumepelekea kupata kivuko ambacho kinawaunganosha na vijiji vingine ingawa msimu wa mvua bado hakipitiki.
"Sisi watu wa ukanda wa tambarare ni kama timesahaulika kabisa lakini tunawashukuru hawa wenzetu wa FT Kilimanjaro kupitia TPC kwa huu ujirani waliofanya kwa kutujengea kivuko lakini nacho bado hakitoshi yunachotaka ni daraja kubwa ili tuweze kuvuka kwenda mashambani na sehemu nyinginezo"alisema
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa Kijiji ni kuwa kutokana na kukosekana kwa mawasiliano ya barabara wakulima wengi wamekuwa wakiuza mazao yao kwa hasara kwani mnunuzi huweka gharama kubwa za kuyatoa shambani hadi barabarani jambo ambalo nalo linazidi kuwaumiza wakulima hao.
"Niwaombe hawa FT Kilimanjaro na TPC kwa ujumla waone umuhimu Sasa wakutujengea daraja ambalo litapitika muda wote ambalo nalo litawezesha hata magari kupitika kirahisi hivyo kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi"alisema
Patrick Mlay ni afisa mtendaji kata ya Arusha Chini ambapo alisema kutokana na kukosekana kwa barabara wakazi wa eneo hilo hulazimika kwenda kupata huduma za matibabu katika wilaya ya Simanjiro wakati ipo hospitali jirani ya TPC lakini ni vigumu kuweza kufika
Alisema kadhalika kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wanaotokea katika ukanda huo ni mdogo kutokana na wengi kutohudhuria masomo hususa kipindi cha mvua kutokana na mafuriko yanayotokea mara kwa mara.
Leonard Waziri no diwani wa kata ya Arusha Chini ambapo alisema alilazimika kutembelea miradi ya ujirani mwema inayotekelezwa na FT Kilimanjaro kupitia TPC ili kuweza kuweka kumbukumbu sambamba na kuwashukuru kwa jitihada wanazozifanya katika kuisadia jamii.
"Nimeona nije kwenye hii miradi ambayo inafadhiliwa na wenzetu wa TPC ili pia niweze kuiambia serikali walichotisaidia na uhitaji wetu kwa sasa ni nini maana kwa kweli hali si nzuri hata kidogo"alisema
Meneja wa FT Kilimanjaro kupitia TPC Kuya Nangai alisema mfuko huo umekuwa ukitekeleza miradi mbali ya kimaendeleo kwa vijiji vinavyozunguka TPC katika nyanja za elimu,afya,kuwasaidia mitaji wajane na kuwajengea uwezo wakulima.
"Kwa sasa sisi TPC hatujafikiria kujenga daraja kama wanakijiji walivyoomba lakini ngoja nilibebe ili mbele ya safari tuone namna ya kufanya maana kazi yetu kubwa ni kisaidia jamii kwenye nyanja mbali mbali"alisema





0 Comments