Ili mtu aweze kufanya uhalifu wowote ule kwanza ni lazima mtu huyo awe na nia ya kulifanya jambo hilo ovu.Mwandishi Adeladius Makwega ,MDTV Mbagala
Pili, akishapata nia au kusudio la kulifanya jambo hilo ndugu huyo atapata au kutafuta pahala/ sehemu/ eneo la kufanya uovu huo.
Tatu, akipatambua pahala hapo ndugu huyu atajiuliza swali je huo uovu ataufanya yeye mwenyewe au kwa shirika?.
Nne, akishatambua hilo anaweza kuufanya uovu huo kwa kutumia mwili au kwa kutumia silaha yoyote ile?(atafanyaje huo uhalifu?). Tano, mhalifu huyo tarajali sasa atafanya uhalifu huo baada ya kuwa na majibu hayo ya masuala yote matano ili kuikamilisha nia yake ovu.
Kwa kutazama maswali hayo natumia herufi P kuyatambulisha ndiyo kuyaita P1, P2, P3, P4 na P5. Sasa, hili kuweza kuzuia uhalifu kama wa wizi au uhalifu mwingine kuna mbinu tofauti unaweza kuzuia tangu kwenye hatua za mwanzo za uhalifu huo.
Wizara yetu ya Mambo ya Ndani ya Nchi chini ya Augustino Lyatonga Mrema ambaye aliiongoza tangu mwaka 1991-1994 ambapo Mkuu wa Jeshi la Polisi alikuwa ni Haruni Mahundi ambaye alikuwa IGP tangu 1984-1996 walifanya kazi kubwa kwa nafasi yao.
Mheshimiwa Mrema alikuwa na dhana ya kupambana na uhalifu katika hatua za awali kama nilivyozitaja.
Jambo hili kwa hakika lilisaidia mno kupunguza uhalifu hasa hasa kwa kutumia polisi jamiii iliyokuwepo nchi nzima kwa kila mtu kulinda eneo lake kwa kutumia sungusungu kila mtaa na kila kijiji.
Kwa sasa kumekuwa na matumizi ya polisi jamii lakini kwa dhana nyingine.
Enzi za Waziri Mrema mhalifu huyo anapokuwa na nia ovu pale anapotaka kwenda kuufanya uhalifu huo tu pale pale akitoka katika nyumba yake alikutana na sungusungu na maswali yalikuwa mengi, wewe ni nani? Unakwenda wapi? Umebeba nini? Au wale waliokwisha fanya uhalifu unatoka wapi na umebeba nini? Kwa hiyo ndiyo kusema uhalifu enzi za Mrema uliweza kuzuiwa katika hatua ya P1, P2, P3 au P4.
Kama uhalifu wa wakati huo ukifikia hatua ya P5 hapo utakuwa umewahusisha watu wengi sana na jambo hilo lilifanya kuweza kujulikana na polisi nao kudhibiti uhalifu huo kwa uwezo na nguvu zote.
Unaweza kuzuia uhalifu katika hatua ya P1 na P2 kwa kuangalia kwa kipi kinasababisha mtu huyo kujihusisha katika huo uhalifu? Kwa mfano umasikini, japokuwa watu wengine ni wahalifu kwa tabia tu.Kwa umasikini kisababisho kinaweza kutatuliwa hasa kwa kutoa ajira kwa jamii hiyo.
Ulinzi wa sungusungu uliratibiwa na wajumbe wa nyumba kumikumi na wajumbe hao walitambua hata tabia za watu wote waliokuwa wakiwaongoza. Kwa mfano katika nyumba moja hadi nyingine kila mmoja alijulikana kwa jina na tabia yake iwe njema au mbaya.
Sungusungu kwa mawazo ya Mrema waliweza kusaidia kwa karibu sana na polisi waliokuwepo katika Vituo Vidogo vya Polisi ambavyo venyewe vilikuwa jirani na makaazi ya raia. Vituo hivyo vidogo vya polisi kama wangeshindwa kupambana na uhalifu huo wangesaidiwa sana na Vituo Vikubwa vya Polisi huku kukiwa na gari za polisi zilizokuwa zikizunguka mitaani.
Ujenzi wa vituo vidogo vya polisi ulikuwa unafanywa na wananchi wenyewe kwa kujichangisha na ujenzi huu ulifanyika kama ujenzi wa shule ya sekondari za kata. Kwa hiyo hapo serikali ilikuwa ikitoa ramani tu na wananchi walijenga chini ya usimamizi wa serikali za mitaa au vijiji na kweli mara vilipomalizika Mheshimiwa Augustino Mrema alifika kuvifungua na kumuagiza RPC wa eneo hilo kupeleka askari polisi na muda mwingine polisi walipelekwa katika vituo hivyo hata kabla mheshimiwa Mrema hajavifungua.
Hoja ya sungusungu na vituo vidogo vya polisi zilikumbwa na upinzani mkubwa kwanza wakisema kuwa sungusungu hawakuwa na ujuzi wa kupambana na wahalifu na polisi ndiyo wenye ujuzi huo wa kupambana na uhalifu.
Wazo la Mrema halikuwa sungusungu kupambana na wahalifu katika ngazi ya silaha tu bali kufanya mapambano na uhalifu katika ngazi za awali kama nilivyodokeza hapo juu P1, P2, na P3.
Japokuwa polisi wamejifunza kupamba na uhalifu, swali ni je wananchi wabweteke na kuwaacha wahalifu kuwasubiri polisi waje kupambana nao? La hasha nia ya Mrema ilikuwa kila mmoja wetu awe mlinzi wa taifa hili pahala tulipo.
Lakini pia polisi ni binadamu kama mimi na wewe wenye nyama na mifupa na panapotokea matukio ya uhalifu mkubwa huwa wanapata madhara na kupoteza maisha. Hakuna mwenye mwili wa chuma. Ndiyo kusema ulinzi ni ushirikiano kwa raia wote iwe askari polisi na mimi na wewe.
Ukija katika dhana pili ya Mrema ya ujenzi wa vituo vidogo vya polisi ambao kwa sasa haupigiwi chapuo sana kumekuwa madai kuwa wananchi walishiriki kwa sehemu kubwa kutoa fedha na rasimali zao. Wapo wanaodaia kuwa baadhi ya watendaji ndani ya Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi yetu wakati huo hili waliliona kuwa kama vituo hivyo vingejengwa kwa kasi basi bajeti ya Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi ingepungua na kupunguza kasi ya ujenzi vituo bora na vikubwa vya Polisi.
Hoja za kuwa vituo vidogo vinaweza kuvamiwa na wahalifu ikashika kasi huku kukitolewa mfano wa matukio hayo ya uvamizi wa vituo vidogo na kweli kasi ya ujenzi wa vituo vidogo ikazikwa katika kaburi.
Binafsi nasema wazi kuwa ujenzi wa Vituo Vidogo vya Polisi kama ukiendelezwa unaweza kuwa na manufaa makubwa kwa kumlinda raia na mali zake huku Serikali kuu ikiendeleza ujenzi wa Vituo Vikubwa vya Polisi.
Kama wananchi wakijenga vituo vidogo vya polisi wataona kuwa ni jengo hilo ni mali yao na polisi ni ndugu zao na hata kutoa ushirikiano kwa zaidi na zaidi kwa jeshi hili.
Kwa siku ya leo napigia chapuo sana Uwaziri wa Mambo ya Ndani wa Mzee wetu Augustino Lyatonga Mrema nikiamini kuwa rekodi yake bado haijavunjwa. Nakuombea afya njema Augustino Lyatonga Mrema.
makwadeldaius@gmail.com
0717649257
0 Comments