Header Ads Widget

AH! AH ! AH! AMIMI NIMEMUONA

 



Nilifika hadi ofisi ya iliyokuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo ilikuwa jirani na mitaa posta ya zamani katika ghorofa moja zuri kidogo, pale walipokuwa wizara hii kwani niliweza kutazama ofisi za Posta kwa chini huku nikiona watu wakifungua masanduku yao ya barua, hiyo kama sikosei ilikuwa mwaka 2014/2015. Nilikaribishwa na mazingira ya ofisi yenye vyumba vingi vingi.....NA ADELADIUS MAKWEGA _DODOMA.


Kwanza niliona ofisi ya Idara ya Habari Maelezo, huku nikiona watu kadhaa wakiingia na kutoka katika ofisi hiyo. Mtu pekee ninayemkumbuka kumuona siku hiyo katika ofisi ya hii alikuwa ni Zamaradi Kawawa kwani ninamkumbuka tangu akiwa anatangaza DW Kiswahili na baadaye akiwa Afisa Habari wa Wizara ya Utumishi wakati hiyo pale Magogoni.


Nakumbuka Zamaradi Kawawa alikuwa amevalia blauzi nyeusi na suruali ya rangi ya giza giza huku ikiwa na mistari ya kwenda chini na shingoni akiwa amevalia kitambulisho chenye mkanda wa rangi ya bluu iliyokoza. Viatu alivyovalia mwanahabari huyu vilikuwa ni vya kuchomeka vya mikanda mikanda vyeusi vyenye kisigino cha stuli.


“Jamani twendeni, tumechelewa.” Nilimsikia akisema.


Zamaradi Kawawa alikiwa akiongozana na watu kana kwamba wakitoka au kuelekea katika mkutano hivi. Kwa kuwa walikuwa na kasi walinipita huku macho yangu yaliyokuwa makini yakimsindikiza Bi Kawawa taratibu na hatua zake alizokuwa akipiga zikiambatana milio wa visigino vyake ko,ko, ko… huku akizimaliza kona za wizara yao wakati huo.Nilijisemea moyoni aah ahh Zamaradi huyo. Hata rafiki yangu niliyekuwa naye kando ndugu yangu Donard Carol (alikuwa Mtangazaji wa TBC International) ambaye niliambatana naye katika safari hiyo alisema,


“Ah ah ah na mimi nimemuona.” 


Niliingia katika chumba kimoja hivi, hapa nilikutana na wahusika wa ofisi hii ambao sikuwatambua kazi zao wala majina yao. Niliwasalimu jamani kwema ? Walinijibu vizuri kwema ! Haya ndugu tuwasaidie nini? Niliwajibu kuwa mimi nina shida ya kuingia ofisi ya Naibu Waziri wa WHUSM. Basi ndugu hawa walinipa maelekezo kuelekea mbele kidogo na kukutana na milango kadhaa na kuingia humo. Maana namna zilivyokuwa walikuwa kama na ghorofa tofauti vile.


Nilikaribishwa na baba mmoja ambaye alikuwa ni mrefu, mweusi ana mwili kidogo huku akinikaribisha katika kiti na kuketi. Haya shekhe niambie shida yako? Aliniuliza swali hilo. nikamjibu mimi ni mtumishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania-TBC nina shida ya Kumuona Naibu Waziri, mheshimiwa Juma Nkamia. Shida gani ? nilimjibu shida ya kikazi tu. Wewe ni nani? Nilimueleza kuwa majina yangu lakini pia ni Mwenyekiti wa Wafanyakazi wa TBC.


Msaidizi huyu wa Naibu Waziri aliniuliza kwa nini usimuone Katibu Mkuu? Nilimjibu kwa lugha nyepesi lakini lugha ngumu suala hili siamini kama Katibu Mkuu anaweza kulitatua mara moja bali Naibu Waziri nina imani naye anaweza kulitatua mara moja.


Msaidizi wa Naibu Waziri alishangazwa na majibu hayo lakini hakukatisha huduma yangu ya kumuona mheshimwa, basi alichukua simu yake ya mezani alizungusha nambari za mheshimiwa Naibu Waziri Juma Nkamia na kumueleza juu ya ugeni wangu.


“Aahh huyo bwana mdogo mruhusu nilishazungumza naye.”


Kweli mheshimiwa Juma Nkamia nilizungumza naye siku moja kabla ya kwenda wizarani hapo akinipa ahadi nifike ofisini kwake na ndiyo maana nilifika hapo ofisini na hoja yangu ilikuwa ni ya naibu Waziri Jumaa Nkamia tu. Kwani mheshimiwa huyu nambari zake nilipewa na Sued Mwinyi ambaye ni rafiki yake sana na walifanya naye kazi kwa muda mrefu tangu RTD.


Siku hiyo nilikuwa natamani kumuona mheshimiwa Juma Nkamia kwa kuwa nilikuwa napeleka hoja ya Wafanyakazi wa TBC, kwake mheshimiwa huyu, yeye pale WHUSM wakati huo alikuwa ni mtu pekee ambaye aliwahi kufanya kazi na Shirika la Utangazaji Tanzania TBC tangu enzi za RTD kwa hiyo mambo mengi ya wafanyakazi, mizengwe na siasa za makazini alikuwa anazielewa sana nadhani kuliko hata Katibu Mkuu Bi Siaba Mkinga na Waziri wake kama sikosei mama mmoja ambaye alikuwa akisuka twende kilioni Dkt Fennela Mukangala.


Kukataa kumuona Bi Siaba Mkinga, Katibu Mkuu wa WHUSM haikuwa kumvunjia heshima au waziri wake bali ilikuwa ni imani yangu na imani ya baadhi wezangu walioniangiza kwa niaba ya wafanyakazi. Mambo yaliyokuwemo katika shajara yangu yangepata majibu haraka kutoka kwa mheshimiwa Juma Nkamia.


Kweli Msaidizi huyu wa Naibu Waziri aliniruhusu na kuingia na kumona mheshimwa Nkamia na kwa hakika mazungumzo hayo hayakuwa ya dakika nyingi bali ni tano tu mbili niliongea mimi huku yeye akinukuu ninayoyasema kutoka katika shajara yangu na mara nilipomaliza mheshimiwa huyu akachukua simu na kuongea na aliyekuwa Mkurugenzi wa TBC wakati huo na alimuita Naibu Katibu Mkuu akampa maelekezo ya Serikali kwa ajili ya kutekeleza maagizo yote aliyoyaagiza siku hiyo. Naibu Katibu Mkuu huyo alikuwa ni mama mmoja ambaye leo hii simkumbuki jina lake.


Yote yalikamilika siku hiyo, niliwapigia simu wezangu juu ya maagizo ya mheshimiwa Juma Nkamia walifurahi sana. Nilitoka na kumuaga msaidizi huyo wa naibu Waziri Mkamia na kwenda zangu TBC BH Barabara ya Nyerere kuendelea na kazi. Kwa bahati mbaya sikumuuliza jina msaidizi huyu wa mheshimwa waziri lakini mwaka 2019 nikaja kumfahamu jina la Msaidizi huyu wa Naibu Waziri wa wakati huo kuwa ni Mwl-Francis Songoro ambaye nimeambiwa kuwa mwaka huu anastaafu akiwa ni mtumishi wa WUSM. Nikikutana naye tena ndugu huyu nitamuuliza juu ya Mheshimiwa Juma Nkamia yu wapi?


makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI