Waziri wa Nishati Mh. January Yusuf Makamba amekutana na kufanya
mazungumzo na Makamu wa Rais wa kampuni ya utafutaji na uzalishaji wa
mafuta na gesi asilia ya Equinor (Afrika) Bw. Paul McCafferty.
Viongozi hao wamekutana Oktoba 21, 2021 katika ofisi ndogo za Wizara ya
Nishati zilizopo jijini Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na
viongozi wengine wa Equinor na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC).
Imeelezwa kuwa mazungumzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya majadiliano ya
Mkataba wa Nchi Hodhi (HGA) wa Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia
(LNG) yanayotarajiwa kuanza rasmi Novemba 8, 2021.
Kwenye kikao hicho, Bw. McCafferty amempongeza Waziri Makamba kwa niaba
ya serikali kwa hatua hiyo ya kuanza tena kwa majadiliano ya mkataba huo wa
HGA kwani yatafungua njia kwaajili ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo wa
LNG.
Bw. McCafferty ameeleza kuwa Equinor iko tayari kwa majadiliano hayo na
kuongeza kwamba mradi huo ni moja ya miradi yenye uwekezaji mkubwa
inayotekelezwa na Equinor duniani, hivyo ni majadiliano muhimu katika kuweka
msingi mzuri wa utekelezaji wake.
Equinor ni moja ya wabia wakuu wa utekelezaji wa mradi huu wa LNG ambao
utasimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA). Wabia
wengine ni pamoja na kampuni ya Shell na TPDC kwa niaba ya serikali.
Mradi wa LNG unakadiriwa kuwa wa thamani ya takriban Dola za Marekani bilioni
30 huku ukitarajiwa kutengeneza nafasi za ajira za moja kwa moja 6,000 na zisizo
za moja kwa moja zaidi ya 15,000 kwa Watanzania.
Waziri wa Nishati Mh. January Yusuf Makamba, (Wa tatu kutoka kulia) akiwa katika
picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa Equinor (Afrika) Bw. Paul
McCafferty, Makamu wa Rais na Mwenyekiti Mkazi, Equinor Tanzania AS, Unni
Merethe Skolstad Fjaer (kushoto kwa Waziri Makamba) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika
la Maendeleo ya Petroli (TPDC) Dkt. James Mataragio, mara baada ya kikao kifupi
kilichofanyika Oktoba 21, 2021 katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es
Salaam.





0 Comments