WAKUU wa vikosi vya JWTZ na JKT wametakiwa kuwa wabunifu katika kubuni miradi mbalimbali ya kibiashara ili Kujenga uwezo wa kifedha wa kuhudumia shughuli mbalimbali za Kijeshi ikiwemo Mafunzo ya Vijana. mwandishi wa matukio daima Hamida Ramadhani anaripoti kutokea Dodoma
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jenerali Venance Mabeyo aliyasema hayo jijini Dodoma wakati akizindua kituo cha burudani kilichojengwa na Jeshi la Kujenga Taifa kilichopo katika eneo la Medel East katikati yaJijini la Dodoma.
"Uzinduzi wa kituo hiki kiwe chachu kwa wakuu wa vikosi na wote wenye nafasi ya kufanya maamuzi ya kubuni mikakati yakufikiria miradi ya maendeleo," alisema Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini
Aidha alilipongeza JKT kwa ubunifu wa Kituo hicho na kutaka majengo ambayo bado hayajamalizika kujengwa yaharakishwe ili Ukumbi huo uwe wa mfano hapa jijini Dodoma.
Naye Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajab Mabele alisema Kituo hicho kitawezesha Maafisa, Askari, Watumishi wa Umma na Wananchi wa Dodoma kutumia ukumbi huo katika shughuli zao mbalimbali kama mikutano ambapo shughuli hizo zitawezesha kituo hicho kujipatia fedha zitakazosaidia kuipunguzia Serikali mzigo wa kuhudumia Jeshi hasa katika malezi ya vijana.
Aliongeza kuwa Fedha za ujenzi wa kituo hicho zimetokana na faida ya miradi mbalimbali iliyo chini ya JKT.
0 Comments