Header Ads Widget

WAKULIMA WA PAMBA SIMIYU WAPEWA SIKU TANO(5) KUNG'OA MASALIA YA PAMBA KWENYE MASHAMBA YAO.

 












Na Bahati Sonda , Simiyu.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila ametoa siku 5 kwa wakulima wa pamba Mkoani humo ambao bado hawajang'oa masalia ya pamba kwenye mashamba yao na kwamba watakaoshindwa watachukuliwa  hatua za kisheria.


Kafulila amesema kuwa kuondoa masalia kwenye shamba kwa mkulima wa zao la pamba ni sheria wala siyo hiari na kusema kuwa lazima watekeleze agizo hilo la kisheria mara moja kabla ya ijumaa ya wiki hii.


Kafulila ametoa agizo hilo mapema jana wakati akizungumza na viongozi, wakiwemo watendaji wa kata katika wilaya ya Meatu Mkoani humo kwenye kikao cha kujadili jinsi Mkoa huo utakavyoweza kuzalisha tani laki tano katika msimu mpya wa pamba.


Amesema kuwa kwa mujibu wa sheria inamtaka mkulima wa pamba kila mwaka ifikapo septemba 15 awe ameshaondoa masalia na magugu yote kwenye mashamba yao na kwamba atakayekaidi anatakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kutozwa faini ya shilingi 50,000 au kifungo cha miezi sita au vyote kwa pamoja.


Aidha amewataka watendaji wa kata baada ya muda uliotolewa kuisha kuhakikisha wanachukua hatua kwa mtu yeyote atakayekaidi kutii agizo hilo kwani Mkoa umejidhatiti kuhakikisha unazalisha kiasi hicho cha pamba katika msimu huu.


"Kufika ijumaa ya wiki hii hakuna shamba lolote kubaki na masalia wala magugu na kwa wale watakaokaidi wakamatwe mara moja na kufikishwa mahakamani lazima sheria itekelezwe kwani hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba mtendaji atakayeshindwa atakuwa umeshindwa kutekeleza majukumu yake na atatakiwa ajieleze kwa nini asichukuliwe hatua kali "Amesisitiza Kafulila

 


Katika hatua nyingine Kafulila amewataka watendaji wote ndani ya wilaya hiyo pamoja na maafisa kilimo na ugani kuhakikisha wanawasaidia wakulima ili waweze  kufuata kanuni bora za kilimo cha pamba hivyo kufikia malengo ya mkoa kwa msimu wa 2021/2022 hali ambayo itaifanya nchi kuwa kinara wa uzalishaji wa zao hilo katika bara la Afrika.




"Ni lazima wakulima wawezeshwe kila kitu, elimu na pembejeo kwa wakati na kwa urahisi na kuwa kila mkulima apande kwa vipimo aweke mbolea , kunyunyuzia viuatilifu na kupata mbegu kwa wakati, tutahakikisha mahitaji yote yanapatikana kwa wakulima"alieleza Kafulila




Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Meatu Faudhia Hamidu amesema kuwa tayari ofisi yake imeanza mkakati wa kuhakikisha inatembelea kila kijiji kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima jinsi ya kuhakikisha wanalima kwa kufuata kanuni bora za kilimo cha zao la pamba.


           

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS