Header Ads Widget

VIONGOZI MBALIMBALI WA SERIKALI WILAYANI MULEBA WAKUTANA KUJADILI NAMNA YA KUTUMIA BIL.5.57.

Kikao kimefanyika katika ukumbi wa Nalphin na kuhudhuriwa na Wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba , Madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba, madiwani wakuu wa shule pamoja na viongozi wengine wa serikali ili kujadili kwa pamoja namna ya kutumia bil.57.5. zilizotolewa na serikali  kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu pamoja na afya wilayani humo. mwandishi wa matukio daimaTitus Mwombeki anaripoti kutoka Bukoba.

Akizungumza katika mkutano huo mkuu wa wilaya ya Muleba Toba Nguvila amewasisitiza  Madiwani, Watendaji wa Kata na Vijiji, Wenyeviti wa Vijiji pamoja na viongozi wa Chama kuhakikisha wanashiriki kwa pamoja katika kutekeleza na kufuatilia ujenzi wa miundombinu hiyo ili kuweza kubaini maeneo ambayo kutakuwa na uhujumu ili hatua ziweze kuchukuliwa.

"Lengo la kuwaita hapa nadhani wote tunafahamu kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa fedha, hivyo kama wilaya tumeona ni vema tukawa na mpango mkakati wa pamoja wa utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu na kama viongozi katika maeneo yetu tunao wajibu wa kufahamu kila hatua itakayoendelea na kuwa na uelewa wa pamoja," ameeleza Mhe. Toba Nguvila.

Pia amemtaka  Mkurugenzi Mtendaji pamoja na wataalamu wote kufika katika kila eneo ambalo linatakiwa kujengwa miundombinu hiyo ili kuweza kufanya tathmini ya mahitaji halisi na gharama zitakazotumika wakati wa utekelezaji wa ujenzi.

Sambamba na hilo, amewashauri viongozi wa kisiasa kuwashawishi na kuwahamasisha wananchi ili waweze kushiriki kwani na wao kwa kiwango kikubwa  pia mchango wao ni muhimu katika ujenzi wa miundombinu hiyo.

"Viongozi wa kisiasa nyie ndio wenye watu mnao uwezo mkubwa wa kuwashawishi wananchi kukusanya vifaa kama mawe, mchanga, kokoto ili kusaidia kupunguza gharama za ujenzi na fedha nyingine iweze kutumika katika ujenzi wa madarasa mengine zaidi ya yale tuliyopangiwa".

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndg. Elias Kayandabila amewataka  viongozi kuhakikisha wanatoa hamasa kwa wanachi, kwa kuendelea kujitolea ili fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi huo zitumike ipasavyo na ikiwezekana pia kujenga miundombinu mingine kwani uhitaji bado ni mkubwa.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba Mhe. Magongo Justus amewaomba na kuwashauri wote wanaohusika na utekelezaji wa shughuli za ujenzi wajiandae kusimamia kwa kadri ya maelekezo yanayotolewa na kuwataka viongozi kuhakikisha wanawaita na kuwashirikisha viongozi na watu walio chini yao ili waweze kujua maelekezo ya matumizi sahihi ya fedha hizo.

Naye Mkuu  wa shule ya sekondari Nyailigamba Mwalimu Archad Kashamba ameshauri kuwa ni vyema bidhaa kuchukuliwa  viwandani ili kuweza kupunguza gharama na ameongezea kuwa usimamizi unakuwa mzuri hasa wa vifaa   endapo walimu wa stoo watapewa jukumu hilo kuliko kutumia watu wengine.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI