Na Mwandishi Wetu, Kibaha Pwani.
MAMLAKA ya Dawa na vifaa Tiba [TMDA] mapema leo tarehe 29 Oktoba 2021 imezindua rasmi Kamati ya Wajumbe wapya wa Kitaalamu wa Usalama wa Dawa, Chanjo na bidhaa zingine zikiwemo vitendanishi na tumbaku ambapo kamati hiyo ni ya tano [5] tangu Mamlaka hiyo ianzishwe.
Jukumu la wajumbe hao ni kuhakikisha kwamba masuala ya usalama wa bidhaa husika yanazingatiwa kwa mujibu wa vigezo vya kitaifa na Kimataifa ili kulinda afya ya mlaji.
Awali akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika mjini hapa katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Wauguzi na Wakunga, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Yonah Mwalwisi, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Bw. Adam Fimbo, alisema Wajumbe hao wapya wanajukumu kubwa la kusaidia Mamlaka hiyo hapa nchini ili kutimiza majukumu yake kwa ufanisi.
"Niwapongeze kwa wale wajumbe wapya mliochaguliwa kwenye kamati hii mpya ambayo ni ya Tano tangu Mamlaka ianzishwe. Lakini pia nizipongeze kamati zote zilizopita kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika ili kulinda afya ya Watanzania.
Kamati hii huundwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura ya 219 ikiwa na jukumu kubwa la kuishauri na kuisaidia Mamlaka katika kuzingatia masuala ya usalama wa bidhaa.
Kamati hiyo ina wataalamu waliobobea katika tasnia ya dawa na vifaa tiba ambao ni maprofesa, madaktari bingwa na wataalam wa tasnia ya dawa waliobobea ambapo idadi ya ni wajumbe 16 na watadumu kwa miaka mitatu.
Dkt. Mwalwisi alisema kuwa, Kamati kuhakikisha mifumo yote ya usalama wa bidhaa zinazodhibitiwa inaimarishwa, taarifa za maudhi ama madhara zinapatikana kwa wakati ilikufanyiwa tathmini ya kina na kusaidia kutoa maamuzi.
" …Ni tegemeo langu kwamba kamati hii itasaidia sana katika kuhakikisha mifumo ya ufuatiliaji inaimarika zaidi, pamoja na kwamba utaratibu wa kufuatilia usalama wa dawa, chanjo kwenye soko ulianza tangu mwaka 2003 na imeendelea kufanyika hadi sasa.
"Takwimu zinaonyesha kuwa bado mwamko wa wataalam wa afya na wananchi kwa ujumla katika kutoa taarifa juu ya madhara ya bidhaa tiba ni mdogo na hivyo taarifa chache zinafika TMDA ikiwa ni wastani wa ripoti 6,000 hadi 8,000 kwa mwaka.
"Kiasi hiki ni kidogo ukilinganisha na idadi inayopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kukusanya angalau ripoti 200 kwa wakazi (inhabitants) milioni 1 kwa mwaka. Hivyo kwa idadi ya watu milioni 60 walioko katika nchi yetu, inatakiwa tuwe tunakusanya ripoti 12,000 kila mwaka ili kutoa uthibitisho wa kisayansi (evidence) juu ya usalama wa bidhaa tiba na kuchukua hatua stahiki." Alisema Dkt. Mwalwisi.
Dkt. Mwalwisi aliongeza kuwa, kutokana na idadi hiyo ndogo ambayo haifikii kiwango kinachohitajika, TMDA imekuwa ikifanya mafunzo na uhamasishaji
Aidha, Dkt. Mwalwisi aliishukuru Kamati iliyomaliza muda wake kwa kufanya kazi nzuri ya kufikisha katika hatua iliyopo sasa ambapo taarifa zikaweza kuongezeka kutoka 300 hadi wastani wa 6,000 hadi 8,000 kwa mwaka.
"Ni matarajio yangu kwamba Kamati hii inayoanza majukumu yake leo, itafanya kazi vizuri zaidi na hatimaye tuweze kufikia malengo yaliyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Pia tunawashukuru sana Taasisi isiyo ya Kiserikali MTaPs – MSH kwa msaada wa kifedha na kuwezesha mafunzo kwa wajumbe wapya wa kamati na utekelezaji wa uzinduzi wa kikao cha Kamati hii vilevile nashukuru kwa kuweza kutupatia ushauri wa kitaalam". Alimalizia Dkt. Mwalwisi.
Nae Mkurugenzi Mkazi wa miradi wa programu ya dawa, ufundi na huduma za maabara kutoka [MSH] iliyochini ya Shirika la Kimataifa la USAID kupitia mradi wa [MTaPS], Dkt. Edger Lusaya alisema wao kama wadau wameweza kutoa msaada wa kifedha wa kuweza kuandaa na kuwezesha mafunzo hayo kufanyika ili kusaidia juhudi za Serikali katika kuimarisha afya ya wananchi wake.
---Mwisho----
0 Comments