Halmashauri za Mkoa wa Kigoma zimeagizwa kuunda sheria ndogo ndogo sitakazosaidia kulinda na kutunza mazingira.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa Thobias Andengenye wakati akizindua kampeni ya upandaji miti kwa kata za Kajana na Mgela zilizopo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma kwa lengo la kulinda vyanzo vya maji na kuondoa uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu kama kilimo, ufugaji pamoja na ukataji miti katika vyanzo vya maji.
"Wananchi,watendaji na viongozi wote wanalo jukumu la kutunza mazingira hivyo basi kila halmashauri kupitia wataalam wake kwa kushirikisha wadau wa maendeleo iendelee kutoa elimu na kuhamasisha upandaji wa miti kulingana na majira kuanzia ngazi ya kaya hadi vitongoji na ziunde sheria ndogo ndogo kusimamia zoezi hilo" Amesema Andengenye.
Andengenye alisema, kila halmshauri ihakikishe kuna uanzishwaji wa mashamba ya miti, na hamasa za upandaji miti zianzie mashuleni kwa kila mtoto kuwa na mti atakaouhudumia.
"Kama jamii, mashirika na wadau mbalimbali wa maendeleo tusipochukua hatua na kuweka mikakati ya kutunza mazingira na uoto wetu wa asili basi ipo hatari kubwa inayoweza kuikumba dunia na kuathiri maisha ya mwanadamu" amesisitiza Andengenye.
Akikabidhi miti zaidi ya milioni moja aina ya Msindano (Pine) katika kijiji cha kajana Mkurugenzi wa Taasisi ya TUUNGANE inayojihusisha na uhifadhi mazingira na afya Lukindo Hiza amesema, mradi huo wa upandaji miti ulihusisha miti ya matunda,biashara na vitalu vya michikichi kwa mikoa ya Kigoma na Katavi.
Amesema kuwa TUUNGANE inafanya hayo ikiwa ni utekelezaji wa sehemu ya ilani ya chama cha mapinduzi, kipengele cha 69 kifungu G ambacho nchi ilihidi ikipewa mamlaka ya kuongeza dola itasimamia serikali kupanda miti.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Kajana Adrian Gwitangira amesema, wananchi waendelee kuhamasishwa kutunza mazingira kwani hata kwa mradi huo walihusika katika shughuli za umwagiliaji na kusimamia mazao hayo ya miti.
Mwisho
0 Comments