Header Ads Widget

TMA YATOA TAHADHARI NA USHAURI KWA MVUA ZA MSIMU NOV 2021 HADI APRIL 2022

Na Fatma Ally MDTV Dar es Salaam

Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania imewashauri watumiaji wa taarifa mbalimbali za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, Wafugaji, mamlaka za wanyamapori mamlaka ya maji na afya waendelee kutafuta kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika Sekta husika.

Wito huo umetolewa kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya, sekta binafsi pamoja na menejimenti za maafa.


Aidha, wadau wanashauriwa kuwasiliana na mamlaka Ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu Ili kukidhi mahitaji maalum katika Sekta zao.


Mamlaka ya hali ya hewa imetoa dondoo muhimu za mvua za Msimu (Novemba, 2021 – Aprili, 2022) ambapo zimelenga kutoa ushauri na tahadhari kwa wadau wa Sekta husika kama ifuatavyo


Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (kanda ya magharibi, kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo yaliyoko kusini mwa mkoa wa Morogoro) katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2021 hadi Aprili, 2022. 


a) Mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka: 

(i)   Mvua zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya na Iringa. Aidha, mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara na kusini mwa mkoa wa Morogoro.


(ii) Vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kati ya mwezi Novemba, 2021 na Januari, 2022. Hata hivyo, ongezeko kidogo la mvua linatarajiwa mwezi Machi 2022.


(iii) Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2021 katika maeneo mengi na kuisha kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Aprili, 2022.


b) Athari na ushauri

(i) Upungufu mkubwa wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi yanayopata mvua za Msimu na kuathiri ukuaji wa mazao. 


(ii) Kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini kinatarajiwa kupungua hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani. 


(iii) Mlipuko wa magojwa unatarajiwa kujitokeza kutokana na upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama

Kwa taarifa zaidi tafadhali tembelea tofuti ya mamlaka www.meteo.go.tz

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI