Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imedhamiria kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anakuwa
na anwani za makazi ifikapo mwaka 2022.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula katika semina ya kujenga
uelewa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa ya Tanzania Bara kuhusu utekelezaji wa
mfumo wa anwani za makazi.
''Tunatarajia kufikisha mawasiliano mpaka vijijini, tunataka nchi nzima iwe na anwani
ya makazi'', amedokeza Dkt. Chaula.
Aidha, amehabarisha kuwa baadhi ya faida za kuwa na anwani za makazi ni
kurahisisha ukusanyaji kodi, kuwezesha biashara mtandao na kuimarisha ulinzi na
usalama.
Awali, akifungua semina hiyo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Prof. Riziki Shemdoe amesema Serikali za Mikoa zina majukumu
ya kusimamia utekelezaji wa anwani za Makazi kwenye maeneo yao
''Serikali yetu ya Tanzania kupitia Sera ya Posta ya mwaka 2003 imeimarisha
mifumo ya anwani za makazi inayoundwa na barabara, njia na namba za nyumba'', amebainisha.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Mary Makondo amesisitiza ushirikiano ili kufikia malengo kwa kuwa moja ya
manufaa ya anwani hizo ni kuwezesha na kufanikisha utambuzi wa majengo na
viwanja vilivyopo ili kurahisisha kazi ya mipango miji na utekelezaji wa majukumu ya
kiuchumi na kijamii kwa Serikali na wananchi kwa ujumla
''Naamini tutaendelea kushirikiana katika kujenga nchi yetu na kuwahudumia
Watanzania'', ametanabaisha Makondo
Ibara ya 61(m) ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025
inaielekeza Serikali iliyopo madarakani kuhakikisha anuani za makazi zinawekwa
nchini ili kurahisisha upatikanaji, utoaji na ufikishishaji wa huduma mbali mbali kwa
wananchi.





0 Comments