MKUU wa Mkoa wa Lindi Bi Zainab Telack amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi Mkoani humo Juma Mnwele kuhakikisha anaweka mazingira na utaratibu wezeshi kwa Wafanyabiashara na wajasiliamali kutumia fukwe za Bahari zilizopo ndani ya Manispaa hiyo kufanya Biashara Usiku na Mchana ili kukuza Uchumi Wao. mwandishi wetu wa matukio daima Hadija Omary anaripoti kutoka Lindi
Telack ametoa agizo hilo jana alipokuwa anazindua mpango wa Kukuza fursa za biashara za Ufukweni kupitia tamasha la michezo Michezo mbalimbali kwa vikundi vya wajasiliamali vya kuweka Akiba ya fedha na kukopa ( VICOBA) lililopewa jina la VICOBA FUN DAY.
Alisema anafahamu changamoto alizonazo Mkurugenzi ndani ya manispaa hiyo lakini swala la kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiliamali hao ni muhimu kwani ni njia moja wapo ya kukuza kipato wa wananchi wao pamoja na kukuza uchumi wa Manispaa hiyo kwa ujumla.
" mimi nataka niwaambie Lindi tunacho kila kitu kinachotakiwa mfano hapa penyewe ni uchumi tosha, kwanini watu wanakwenda kwenye fukwe za Coco kule Dar es salaam ukifika pale mihogo ya kukahanga , ya kuchemsha mara samaki waliotoswa , waliofanywa nini hivyo vyote Lindi vipo ni swala la kujipanga tuu" alisema Telack.
"Nakuagiza Mkurugenzi kwenye Eneo hili naomba litumike Mchana pia litumike usiku kuna zile taa naziona Barabarani ndio maana watu wanakaa kule hebu fanya fikra tafuta taa kama tano uje kufunga hapa hawa wananchi waburudike wale upepo wa Pwani" aliongeza Telack
Aidha aliongeza kuwa katika kipindi hiki ambacho Serikali ipo katika mpango kabambe wa kufungua fursa Nchini, tamasha hilo litatumika katika kuelekea kwenye mikakati mikubwa ya kufungua uchumi ndani ya Mkoa huo wa Lindi.
Kwa upande wake mmoja wa wanawake wa kikundi kiitwacho Tuwe pamoja, aliushukuru uongozi wa Mkoa huo kwa kuwafungulia wajasiliamali hao fursa hiyo ya biashara pia aliuomba uongozi huo kufanya tamasha hilo kuwa Endelevu kufanyika mara kwa mara ndani ya Manispaa hiyo .
Awali Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga alisema kuwa Baada ya uzinduzi huo sasa Tamasha hilo litakuwa Endelevu kwa siku zote za Mwisho wa wiki kwa wajasiliamali kufanya biashara katika Maeneo hayo ya Fukwe za Bahari huku akieleza kuwa huo utakuwa ni mwanzo mzuri wa kufungua Mkoa wa Lindi pamoja na uchumi wa Mtu mmoja mmoja.





0 Comments