RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Oktoba 23 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) yatakayofanyika Ikwiriri Rufiji.
Aidha sherehe hizo zinaadhimishwa wilayani Rufiji ili kumuenzi Bibi Titi Mohamed ambaye wazazi wake ni wazaliwa wa wilaya hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Kibaha mwenyekiti wa UWT Taifa Gaudentia Kabaka alisema kuwa wiki hiyo itaambatana na kutoa misaada mbalimbali mashuleni na wagonjwa kwenye hospitali ya Wilaya.
Kabaka alisema kuwa wameamua kumualika Rais ambaye ni mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni mwanamke ameonyesha ubunifu mkubwa katika kuwaletea wananchi maendeleo.
"Tumemwalika Rais ili tumpongeze kwanza ni mwanamke mwenzetu na ameonyesha kufanya mambo makubwa ndani ya nchi na ameonyesha ushupavu na ubunifu na kushawishi wafadhili,"alisema Kabaka.
Alisema kuwa ubunifu huo umewezesha Tanzania kupata fedha kiasi cha shilingi trilioni 1.3 ambazo zinatokana na Covid-19 ambapo zinapelekwa kwenye miradi ya maendeleo.
Naye mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge alisema kuwa ushujaa wa Rais ni wa kuungwa mkono ambapo anaonyesha kuwapigani wananchi.
Kunenge alisema kuwa katika mpango wa maendeleo kupitia fedha za covid-19 mkoa huo utapata kiasi cha shilingi bilioni 13 ambapo kwa fedha za miamala vitajengwa vituo vya afya na zahanati kwenye wilaya tano.





0 Comments