Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewahimiza wadau wa michezo nchini kujenga tabia ya kushiriki michezo mbalimbali hasa mbio za marathon zinazoandaliwa kwa nyakati tofauti tofauti.
Alisema hayo jana baada ya kumalizika kwa Mashindano ya Mbio za Rock City Marathon yaliyofanyika jijini Mwanza.
“Kushiriki katika mashindano kama haya hakusaidii tu kupata zawadi mbalimbali bali ni njia mojawapo ya kuimarisha afya ” Masanja alisema.
Aliongeza kuwa mashindano ya mbio za marathon yatasaidia kuhamasisha utalii, kukuza pato la mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla kutokana na washiriki kuchangia katika kulipia huduma mbalimbali za malazi, vyakula nk.
Aidha, Masanja alisema Wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa sekta binafsi inayoandaa mashindano kama hayo na amewaelekeza watendaji kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya mashindano ya mbio za Marathon mara yanapojitokeza.
Katika mashindano hayo, Mary Masanja alikabidhi zawadi na medali kwa washindi wakiongozwa na Mwanariadha wa Kimataifa kutoka nchini Tanzania Alphonce Simbu aliyeibuka mshindi wa kwanza kwenye mbio za kilomita 21 kwa upande wa wanaume, akifuatiwa na mshiriki kutoka Kenya Benard Musau.
Kwa upande wa wanawake katika mbio za kilomita 21 ziliongozwa na Isgani Chameo kutoka Kenya akifuatiwa na Neema Msuhadi na Tunu Andrew kutoka Tanzania.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala alisema kuwa mbio hizo ni nyenzo muhimu ya kuwaandaa wanariadha nchini kuwa katika nafasi ya kufanya vizuri katika michuano ya Kimataifa itakaoipa heshima nchi ya Tanzania.
Naye Mratibu wa Mashindano hayo Kasara Naftal alisema kuwa mbio hizo zimefanyika kwa mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano alioupata kutoka kwa uongozi wa Mkoa wa Mwanza, Shirikisho la Riadha Taifa, Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza na wadhamini mbalimbali.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akivishwa medali na Mratibu wa Mashindano ya mbio za Rock City Marathon, Kasara Naftal katika mashindano ya mbio za Rock City Marathon zilizofanyika jijini Mwanza.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Ludovick Nduhiye akimpa mkono wa pongezi mshindi wa pili wa mbio za kilomita 21 kwa upande wa wanawake Neema Msuhadi katika mashindano ya mbio za Rock City Marathon zilizofanyika kwenye jijini Mwanza. |
0 Comments