Header Ads Widget

MUHIMBILI YAPITIA UPYA MWONGOZO WA UPANDIKIZAJI FIGO KUBORESHA UBORA WA HUDUMA


Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepitia upya Mwongozo wa Utoaji Huduma za Upandikizaji Figo (Standard Operating Procedures – SOPs), uliokuwa ukitumika kwa miaka tisa tangu kuanza kwa huduma hizo mwaka 2017. Zoezi hilo limewakutanisha wataalamu wa upandikizaji figo kwa lengo la kuhuisha mwongozo huo ili kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba duniani, kuimarisha usalama wa wagonjwa na kuboresha viwango vya utoaji huduma.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi hicho, Dkt. Juma Mfinanga, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, amepongeza hatua zinazochukuliwa na hospitali katika kuendeleza huduma za upandikizaji figo, hususan matumizi ya teknolojia na mbinu za kisasa za upasuaji. Ameeleza kuwa juhudi za wataalamu katika kupitia upya mwongozo huo ni sehemu muhimu ya kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora, salama na zinazozingatia maendeleo ya kitaalamu. Pia amewapongeza kwa kuandaa kikao hicho na kuwasisitiza kudumisha mshikamano, ushirikiano na upendo katika utendaji kazi. “Huduma za upandikizaji figo zinahitaji ushirikiano wa karibu wa wataalamu kutoka kada mbalimbali. Ni muhimu kuendelea kushirikiana, kusaidiana na kufanya kazi kama timu ili kuiendeleza Muhimbili na kuendelea kupeperusha bendera ya ubora katika huduma za upandikizaji figo,” amesema Dkt. Mfinanga.

Hospitali ya Taifa Muhimbili ilianza kutoa huduma za upandikizaji figo mwaka 2017, na tangu wakati huo zaidi ya wagonjwa 100 wamefaidika na huduma hiyo. Aidha, hospitali imeendelea kuboresha teknolojia na mbinu za matibabu, ambapo kwa sasa upandikizaji figo unafanyika pia kwa kutumia mbinu ya upasuaji wa matundu madogo (Minimally Invasive Surgery), inayowezesha utoaji wa huduma kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya upasuaji.

Kupitia maboresho ya mwongozo huo, MNH inalenga kuhakikisha huduma za upandikizaji figo zinaendana na viwango na maendeleo ya kisayansi duniani, huku zikizingatia ubora, usalama na mahitaji ya wagonjwa. Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, hospitali inaendelea kuimarisha huduma hizi na kupanua fursa za matibabu kwa wagonjwa wenye uhitaji nchini Tanzania.










Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI