Header Ads Widget

KAMISHNA MWISHAWA: ENDELEENI KUDHIBITI UJANGILI ILI KUBORESHA UHIFADHI WA MALIASILI ZA TAIFA



Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Mwishawa, leo Novemba 4, 2026, amewataka Maafisa na Askari Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato kuendeleza juhudi za kudhibiti ujangili ili kulinda maliasili za Taifa ziweze kudumu kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. Kamishna Mwishawa aliyasema hayo wakati wa kikao na Maafisa na Askari hao , kikao kilichofanyia katika Ofisi ya Makao Makuu ya Hifadhi yaliyopo Biharamulo Mkoani Kagera.

Aidha, Kamishna Mwishawa alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mahusiano na ushirikiano kati ya hifadhi na jamii zinazozunguka hifadhi kwa kujenga uelewa mpana kuhusu umuhimu wa uhifadhi, kuwashirikisha wananchi katika kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha jamii zinanufaika na uwepo wa hifadhi. Vilevile, aliwahimiza kuzingatia weledi, uadilifu, nidhamu na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Sambamba na hilo, Kamishna Mwishawa amewaasa Maafisa na Askari Uhifadhi wa hifadhi hiyo kuwa wazalendo na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele huku wakijiepusha na vitendo vilivyo kinyume na maadili ya utumishi wa umma ikiwemo rushwa. 

Akizungumza kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Godwell Ole Meing'ataki ambaye ndiye Mkuu wa Kanda ya Magharibi, alisisitiza kuwa Shirika linaendelea kuboresha upatikanaji wa magari na ndege nyuki (drones), pamoja na kutoa mafunzo kwa watumishi ili kuongeza ufanisi katika shughuli za uhifadhi, doria na mapambano dhidi ya ujangili.

Naye, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Halid Mngofi, aliushukuru uongozi wa Shirika kwa kutembelea hifadhi hiyo, akieleza kuwa ziara hiyo imeongeza morali na ari ya watumishi katika kutekeleza majukumu yao kwa bidii na weledi. Aidha, aliahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Kamishna wa Uhifadhi.

Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato ni hifadhi ya kipekee inayopatikana katika Mkoa wa Geita na Kagera, ikijivunia kuwa na mandhari ya kuvutia, wanyamapori, utajiri wa bioanuwai na fursa mbalimbali za utalii wa ikolojia.







Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI