NA FARIDA MANGUBE MATUKIO DAIMA MEDIA
Wakala wa Nishati Vijijini REA imejipanga kuendelea kuimarisha na kuwezesha Waendelezaji wa Miradi Midogo ya Kuzalisha Umeme kwa Maporomoko ya Maji, ikiwemo kuhakikisha miradi hiyo inalindwa dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Nino zinazotarajiwa kunyesha katika kipindi hiki.
Kauli hiyo imetolewa leo Oktona 6, 2026 na Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala wa REA, Mhandisi Advera Mwijage, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Umeme wa Ijangala wenye uwezo wa kuzalisha Kilowati 360, uliopo katika Kijiji cha Masisiwe, Wilaya ya Makete mkoani Njombe.
Mhandisi Mwijage amesema REA imewafikishia waendelezaji wadogo wa miradi ya uzalishaji umeme wa maji maelekezo ya kuchukua tahadhari, ikiwemo kujenga na kuimarisha miundombinu ya kupitisha maji ili kuzuia uharibifu wa mitambo wakati wa mvua kubwa.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mwijage, ziara hiyo pia imelenga kuona namna Mradi wa Ijangala unavyoendelea kuzalisha umeme, ambapo amesema REA imefarijika kuona uzalishaji ukiendelea vizuri.
Amesema matumizi ya rasilimali za maji kwa ajili ya kuzalisha umeme ni miongoni mwa njia muhimu za kuongeza upatikanaji wa umeme nchini, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kutunza vyanzo vya maji na kuepuka shughuli zinazoweza kuharibu mazingira.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Umeme wa Ijangala, Daudi Sanga, amesema mradi huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na mchango wa REA, ikiwemo fedha zilizotolewa kama ruzuku na kuwezesha upatikanaji wa fedha za mkopo kupitia Benki ya Maendeleo ya Tanzania TIB.
Sanga amesema mradi huo umepokea zaidi ya shilingi bilioni 1.4 kutoka REA, huku pia akieleza kuwa kupitia utaratibu wa REA na TIB, mradi ulipata mkopo wa takribani Dola Laki Nne za Marekani, fedha zilizosaidia kukamilisha ujenzi wa mradi huo.
Katika kukabiliana na mvua kubwa zinazotarajia kuanza kunyesha hivi karibuni, Sanga amesema wameanza kuchukua hatua za kulinda bwawa, mtambo na miundombinu mingine ya mradi, ikiwemo kuandaa mfumo wa kuzuia magogo yanayoweza kusombwa na maji kuelekea kwenye bwawa na mitambo.
Amesema baadhi ya maeneo ya kingo yanaendelea kufanyiwa maboresho, huku wakitafuta njia za kudhibiti mchanga unaosombwa na maji ambao unaweza kuathiri utendaji wa mashine za kuzalisha umeme.
Sanga amewataka waendelezaji wengine wa miradi midogo ya umeme wa maji kutozipuuza tahadhari za wataalamu wa hali ya hewa, akisema maandalizi ya mapema yanaweza kuzuia uharibifu mkubwa wa miundombinu na hasara ya fedha zilizowekezwa.
REA imesema itaendelea kushirikiana na waendelezaji wadogo wa miradi ya kuzalisha umeme kwa maporomoko ya maji ili kuongeza uzalishaji wa umeme, kuimarisha upatikanaji wa nishati na kuhakikisha uwekezaji unaendelea kuwa salama hata katika kipindi cha mvua kubwa.








0 Comments