Kampuni ya OpenAI imekiri kuwa hatua ilizochukua "hazikutosha" baada ya mmoja wa mawakala wake wa akili mnemba (AI) kwenda nje ya mipaka iliyowekwa na kuvamia tovuti za serikali ya Australia mwezi Juni.
Afisa Mkuu wa Mkakati wa kampuni hiyo, Jason Kwon, alifika mbele ya kikao cha bunge kuhusu AI mjini Sydney Jumanne, ambapo alisema tukio hilo "halikupaswa kutokea" na kwamba kampuni hiyo "ilipaswa kushughulikia majibu yake kwa njia bora zaidi."
OpenAI ilikosolewa kwa kuchelewa kuijulisha serikali ya Australia kuhusu uvamizi huo. Inadaiwa kuwa ilichukua wiki kadhaa kabla ya taarifa kutumwa, tena kupitia barua pepe kwa kisanduku cha jumla cha mawasiliano badala ya kuwafikia moja kwa moja viongozi wa serikali.
"Tunaomba radhi na tunajua kuwa tuna kazi kubwa ya kufanya ili kurejesha imani ya watu wa Australia," alisema Kwon.
Tukio hilo lilitokea baada ya wakala wa OpenAI kwenda nje ya maelekezo yake na kuingia katika mfumo binafsi wa takwimu uliokuwa na taarifa zisizo nyeti kutoka mpango wa huduma za afya wa taifa wa Australia, Medicare.
Wataalamu wa usalama wa mtandao walieleza kuwa huenda hili likawa tukio la kwanza la aina yake ambapo AI imehusishwa moja kwa moja na uvamizi wa mfumo wa kidigitali.
Alipoulizwa kwa nini OpenAI haikuwasiliana moja kwa moja na mawaziri wa serikali mara tu ilipogundua uvamizi huo, Kwon alikubali kuwa hilo lilikuwa kosa.
"Tuulipaswa kufanya kile mnachopendekeza," alisema, akijibu swali la kamati kuhusu kwa nini kampuni haikupiga simu moja kwa moja kwa viongozi wa serikali.
Wakati huo huo, kampuni pinzani ya AI, Anthropic, nayo ilihudhuria kikao hicho na kusema kuwa uchunguzi wake wa hivi karibuni haukubaini ukiukaji wowote unaohusisha mifumo yake nchini Australia.






0 Comments