Na Elamu Nyaulingo (UOI), Matukio Daima Media, Iringa
HALMASHAURI ya Manispaa ya Iringa inatarajia kutoa mikopo isiyo na riba yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 400 kwa vikundi vya wajasiriamali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wananchi kupata mitaji na kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, alisema hayo alipokutana na wafanyabiashara wa Soko la Mnada, ambapo alieleza kuwa halmashauri inaendelea kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara, ikiwemo ukosefu wa mitaji na maeneo ya kufanyia biashara.
Alisema katika awamu inayofuata ya utoaji wa mikopo hiyo, halmashauri inatarajia kukopesha vikundi zaidi ya 35, vikiwemo vikundi vipya vilivyokidhi vigezo vya kunufaika na mpango huo.
Alisema mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kuendeleza biashara zao kwa kuzingatia mahitaji ya kila mwanakikundi na aina ya shughuli anazofanya.
“Katika kundi hili, tunategemea ndani ya wiki ijayo kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 400. Wanufaika tayari wamepatikana, na ni zaidi ya vikundi 35 tutakavyovipatia mikopo, vikiwemo vikundi vipya,” alisema Mlawa.
Akizungumzia masharti ya mikopo hiyo, alisema utaratibu wa kujiunga na vikundi na kunufaika na mikopo si mgumu kama baadhi ya wananchi wanavyodhani, akisisitiza kuwa mikopo hiyo haina riba.
Alisema halmashauri inaendelea kusajili vikundi vya watu watano, huku kiwango cha mkopo kwa kila mwanakikundi kikizingatia mahitaji ya biashara yake, na kikundi kikiwa dhamana ya mkopo.
“Wengine wamekuwa wakitisha wananchi kwamba mikopo ya Serikali ina masharti magumu, lakini mikopo hii haina riba. Mwananchi anaweza kupata mkopo kulingana na mahitaji ya biashara yake, huku dhamana ikiwa ni kikundi chenu,” alisema.
Alifafanua kuwa mwanakikundi mmoja anaweza kukopeshwa Sh milioni mbili, mwingine Sh milioni tatu, milioni tano au milioni 10, kulingana na mahitaji yake, huku marejesho yakifanywa kwa utaratibu wa kikundi.
Katika hatua nyingine, Mlawa alisema Manispaa ya Iringa inapanga kupanua wigo wa uwezeshaji kwa kutoa mikopo ya vifaa mbalimbali, ikiwemo vifaa vya muziki kwa vijana wanaotaka kuanzisha na kuendeleza shughuli za bendi.
Alisema mpango huo unalenga kupunguza gharama za kukodi vifaa vya muziki na kuwapa vijana fursa ya kutumia vipaji vyao kujipatia kipato.
“Tuliona kuna kundi kubwa la vijana wanaojihusisha na bendi na matamasha, lakini wanakodi vifaa vya watu wengine. Tukaona ni vyema Manispaa ya Iringa iwasaidie kwa kuwakopesha vifaa vitakavyowawezesha kuendeleza shughuli zao,” alisema Mlawa.
Alisema halmashauri pia itakuwa tayari kutumia huduma za bendi zitakazonufaika na mpango huo katika matamasha, makongamano na sherehe zake mbalimbali, hatua itakayowapa vijana fursa ya kupata wateja na kuongeza mapato.
Aidha, alisema halmashauri inaangalia uwezekano wa kutoa mikopo ya magari ya mizigo na abiria kwa vikundi vyenye mahitaji hayo, pamoja na kuwawezesha wafanyabiashara wanaojihusisha na shughuli za usafirishaji, wakiwemo waendesha bodaboda na bajaji.
Mlawa alisema halmashauri tayari imenunua lori lenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 120 kwa kutumia mapato ya ndani, akieleza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa kupanua fursa za kiuchumi kwa wananchi kupitia miradi na mikopo.
Kuhusu changamoto ya ukosefu wa maeneo ya kufanyia biashara, alisema halmashauri itachunguza uwezekano wa kuwapatia wafanyabiashara nafasi katika fremu zilizopo eneo la Mamwimbi kwa gharama nafuu.
Alisema maombi ya wafanyabiashara wanaohitaji maeneo makubwa zaidi yataendelea kushughulikiwa kwa kushirikiana na mamlaka husika ili kupata ufumbuzi unaofaa.
Katika maelezo yake, Mlawa alisema mpango huo unaendana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia shughuli za uzalishaji na biashara.
Aliwataka wafanyabiashara wa Soko la Mnada kuendelea kudumisha umoja, uadilifu na mshikamano, akieleza kuwa ushirikiano miongoni mwao ni muhimu katika kukuza biashara zao na kuchangia maendeleo ya Manispaa ya Iringa.






0 Comments