Header Ads Widget

POLISI DAR YAWAKAMATA 11 KWA HUJUMA MIUNDOMBINU YA TTCL


Na Matukio DaimaMedia 

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watu 11 wanaodaiwa kujihusisha na wizi, uharibifu, usafirishaji na biashara haramu ya miundombinu ya mawasiliano ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa kanda maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro amesema kuwa, Jeshi hilo limesema limefanya operesheni hiyo kwa kushirikiana na kitengo cha usalama cha TTCL baada ya kubaini kuibuka kwa matukio ya wizi na hujuma dhidi ya miundombinu hiyo, likisisitiza kuwa halitamvumilia mtu yeyote anayehusika na uhalifu huo bila kujali umri au hadhi yake.

Akizungumza kuhusu hali ya usalama jijini, Jeshi hilo limesema kwa ujumla Dar es Salaam ni shwari, huku shughuli za kiuchumi, kisiasa na kijamii zikiendelea vizuri.

Amesema kuwa, pamoja na hali hiyo, limeendelea kutoa elimu kwa wananchi katika mitaa, kata, tarafa na wilaya kuhusu masuala ya usalama, likieleza kuwa elimu ni moja ya nyenzo muhimu katika kuzuia vitendo vya jinai, uhalifu na makosa ya usalama barabarani.

Katika suala la hujuma za miundombinu ya TTCL, Jeshi hilo limesema baadhi ya wahusika huenda maeneo mbalimbali na kukata au kuiba nyaya na vifaa vya mawasiliano, huku wengine wakihusika kuvipokea, kuvisafirisha na kuviuza.

Aidha, amesema baadhi ya wahalifu hulenga nyaya zenye shaba (copper), ambayo ina thamani kibiashara, lakini kitendo cha kuiondoa kwenye miundombinu ya taifa kwa ajili ya biashara haramu husababisha madhara makubwa kwa taasisi na wananchi wanaotegemea huduma za mawasiliano.

"Uhalifu hauna rika. Wapo watoto, vijana na watu wazima wanaohusika. Mpokeaji na anayenunua au kuuza mali za wizi unaweza kukuta ni mtu mzima," limeeleza Jeshi hilo.

Aidha, limeonya kuwa baadhi ya watu hujificha nyuma ya shughuli halali kama karakana au biashara nyingine na kutumia maeneo hayo kupokea mali zinazodaiwa kuwa zimeibwa au kuharibiwa.

Sambamba na hilo amesema pia baadhi ya wanaohusika hujifanya kuwa mafundi au wafanyakazi wa kampuni za mawasiliano kwa kuvaa mavazi kama makoti yenye vimulimuli, buti na glovu na kubeba vifaa vya kazi ili wasishtue wananchi wakati wakifanya uhalifu.

Amesema kuwa, Jeshi la Polisi haliwezi kutaja kwa sasa kiasi kamili cha fedha kinachopotea kutokana na wizi huo, lakini limeonya kuwa hasara inayosababishwa na kukatika kwa mawasiliano ni kubwa zaidi ya thamani ya nyaya au vifaa vinavyoibiwa.

Ameongeza kuwa, taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi hutegemea miundombinu ya mawasiliano katika shughuli zao, hivyo inapoharibiwa, huduma na shughuli za kiuchumi zinaweza kuvurugika.

"Gharama ni kubwa, kwa mfano, taasisi kama Muhimbili ikikosa mawasiliano, unajua watu wanapata hasara kiasi gani? Taasisi za Serikali na hata binafsi zinakosa mawasiliano,” limeeleza.

Amesema kuwa, jeshi hilo linachunguza sababu zilizosababisha wahalifu kurejea kwenye miundombinu ya TTCL, baada ya awali matukio ya wizi wa vyuma na vifaa kuelekezwa zaidi katika miundombinu ya taasisi nyingine, ikiwamo TANESCO.

Amesema linaendelea kushirikiana na TTCL katika uchunguzi na ufuatiliaji wa wahusika, huku likifanya kazi mchana na usiku kuhakikisha wanaopanga, kuiba, kupokea, kusafirisha au kuuza miundombinu hiyo wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kwa upande mwingine, Jeshi hilo limekemea vikali hujuma dhidi ya miundombinu ya taifa, likisema mawasiliano ni sehemu muhimu ya uchumi, siasa na maisha ya kijamii, hivyo uharibifu wake unaweza kuathiri shughuli za taasisi nyingi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI