Moshi
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imezishauri taasisi na mashirika ya umma kutanguliza uzalendo na maslahi ya umma kwa kutumia fedha za walipa kodi kununua bidhaa za ngozi zinazozalishwa ndani ya nchi.
Ushauri huo umetolewa na wajumbe wa kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Hawa Mchafu wakati wa ziara ya kikazi waliyoifanya kukagua mradi wa kiwanda cha Ngozi cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KLICL) leo (13 Machi 2026) mjini Moshi.
Wakiwa kwenye kiwanda hicho, Kamati ya bunge ilijulishwa kupitia taarifa iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu kuwa licha ya kiwanda kuanza uzalishaji mwaka 2017 na kuzalisha bidhaa bora za ngozi bado kuna changamoto ya soko la ndani la bidhaa hizo.
Waziri Sangu alibainisha kuwa kiwanda hicho kinachomilikiwa na Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Jeshi la Magereza imewekeza zaidi ya shilingi Bilioni 142 hadi kukamilika kwake.
“Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha hadi jozi milioni 1.2 za viatu kwa mwaka, soli za viatu jozi milioni 2.1 kwa mwaka, bidhaa mbalimbali za ngozi (leather articles) kama vile mikanda, mabegi, pochi, makoti (leather jackets) n.k zipatazo 184,500 kwa mwaka” alisema Waziri Sangu.
Wakizungumza baada ya ukaguzi wa kiwanda hicho Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge Hawa Mchafu aliishauri Wizara pamoja na Menejimenti ya kiwanda cha KLICL kuwa na mkakati mahsusi wa kutangaza bidhaa za ngozi ili zivutie masoko.
Mwenyekiti huyo alipongeza kiwanda hicho kwa kuzalisha ajira za watanzania ambapo ametaka jitihada zaidi za kutangaza bidhaa zake kwa kutumia jina la Tanzania.
Kwa upande mjumbe wa kamati hiyo Lucy Kombani na Kafiti W. Kafiti walipongeza jitihada za Mfuko wa PSSSF kwenye uwekezaji wa kiwanda hicho na kushauri serikali ihamasishe taasisi zake kufanya manunuzi ya bidhaa za ngozi ikiwemo viatu kwenye vyombo vya ulinzi na usalama pia shule kutoka kiwanda hicho.
Kamati hiyo ya Bunge inaendelea na ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira na Mahusiano ambapo kesho itatembelea mradi wa kiwanda cha chai Mponde kilichopo Lushoto mkoani Tanga.
Mwisho







0 Comments