Header Ads Widget

PROF. SILAYO ASISITIZA NIDHAMU YA FEDHA NA USHIRIKIANO KATIKA UCHAMBUZI WA BAJETI YA TFS 2026/2027

Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo


Morogoro:

Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, amewataka wahifadhi wa TFS kuzingatia nidhamu ya matumizi ya fedha na kuandaa mipango yenye tija ili kuhakikisha Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 inaleta matokeo chanya kwa taasisi na Taifa kwa ujumla.

Akifungua kikao cha Uchambuzi wa Mpango na Bajeti kilichofanyika Februari 24, 2026 katika Ukumbi wa Hoteli ya Cate, mkoani Morogoro, Prof. Silayo alisema upangaji wa bajeti unapaswa kuzingatia uhalisia wa mapato na matumizi sambamba na malengo ya kimkakati ya TFS.

Alisisitiza kuwa watumishi wanapaswa kusimamia kwa makini rasilimali za umma, kuepuka matumizi yasiyo na tija na kupunguza mabadiliko ya bajeti yasiyo ya lazima katikati ya mwaka wa fedha.

“Tunapanga bajeti kwa kuzingatia malengo mahsusi. Kila fedha itumike kutekeleza vipaumbele vilivyopangwa na kuleta matokeo yanayopimika,” alisema Kamishna.

Prof. Silayo aliagiza kila kanda na kitengo kuainisha kwa uwazi vyanzo vya mapato, fursa zilizopo na mikakati ya kuvitumia bila kuathiri misitu ya asili, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mashamba ya miti na kubuni miradi yenye tija.



Aidha, aliwataka wakuu wa vitengo kuhakikisha miradi inayoanzishwa inakamilika kwa wakati na kuepuka kuacha miradi njiani kutokana na upangaji dhaifu au usimamizi usioridhisha.

Kamishna alikumbusha kaulimbiu ya taasisi ya “Timu Moja, Dira Moja,” akisema mafanikio ya bajeti hiyo yatategemea mshikamano, uwajibikaji na ushirikiano wa watumishi wote.

Awali, Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia Masoko na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu, Salehe Beleko, alisema bajeti ya 2026/2027 inaandaliwa sambamba na kukamilika kwa Mpango Mkakati wa Nne (SP4) wa miaka mitano, utakaokuwa dira ya utekelezaji wa taasisi. Alibainisha kuwa mchakato wa maandalizi ulianza Desemba mwaka jana na ulikuwa shirikishi, ukihusisha vituo, mashamba, kanda na idara mbalimbali.

“Tumelenga kuwa na bajeti itakayorekebisha changamoto za nyuma, kupunguza fedha zisizotumika na kuongeza tija katika utekelezaji,” alisema Beleko.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI