Header Ads Widget

MEJ. JEN (MST) SEMFUKO AWAVISHA VYEO VYA KIJESHI MAKAMISHNA WA UHIFADHI 13


Na. Joyce Ndunguru, Morogoro.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mej.Jen (Mst) Hamis Semfuko amewavisha vyeo vya kijeshi Makamishna wa Uhifadhi (13) katika hafla ya Kijeshi iliyofanyika Februari 21, 2026, katika Ofisi za TAWA Makao Makuu, Mkoani Morogoro.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mej.Jen (Mst) Semfuko aliwapongeza Makamishna kwa kuaminiwa na Bodi ya Wakurugenzi na kuteuliwa nafasi hizo katika maeneo mbalimbali ya usimamizi.

“Ninawapongeza Makamishna wote 13 waliotunikiwa na kuvishwa vyeo, ni imani ya Bodi kuwa mnastahili vyeo hivyo, hongereni sana,” alisema Mej.Jen (Mst) Semfuko.




Aidha, pamoja na pongezi hizo, Semfuko aliwaelekeza Makamishna waliovishwa vyeo kwenda kutekeleza maelekezo ya Serikali na maono ya Bodi ya nne ya Wakurugenzi ya TAWA ya kuhakikisha TAWA inapaa katika viwango vyote vya utendaji kazi ikiwemo; ushirikishaji wa jamii, usimamizi wa kazi za uhifadhi, kuendeleza Utalii, kuongeza uwekezaji na ukusanyaji wa mapato. 

“Tunataka tuone TAWA inapaa juu zaidi na nyinyi ndio moja ya vichocheo vya kufanya hivyo,” alisema Semfuko.

Kadhalika, Mej.Jen (Mst) Semfuko aliwataka Makamishna wa uhifadhi kwenda kufanya kazi kwa kushirikiana na Maafisa na Askari walio chini yao kwa kuzingatia miongozo iliyopo huku wakizingatia ubunifu, weledi, sheria na utu.

Makamishna wa Uhifadhi waliovishwa vyeo ni pamoja na Makamishna Wasaidizi Waandamizi (7) ambao ni Privatus Kasisi, Wilbright Munuo, Khadija Malongo, Mark Chuwa, Vicky Kamata, Omary Msangi na Orest Njau. 

Pia, Makamishna Wasaidizi (6) ambao ni Alphonce Mung’ong’o, Jackson  Msaki, Suleiman Keraryo, Jovine Nachihangu, George  Makheya na Rajabu Hochi.














Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI