Header Ads Widget

MAANDALIZI YA UZINDUZI WA UWANJA WA NDEGE WA MTEMERE YAPAMBA MOTO, DKT. ABBASI ARIDHISHWA NA UKAMILISHAJI WA MIRADI


Na. Philipo Hassan, Hifadhi ya Taifa Nyerere.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, leo Februari 09, 2026, amefanya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Hifadhi ya Taifa Nyerere, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mtemere. Dkt. Abbasi ameridhishwa na hatua za ukamilishaji wa miradi hiyo ambayo imeshakamilika na inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba mapema Februari, 2026.

Dkt. Abbasi aliipongeza TANAPA kwa kusimamia ujenzi wa miradi hiyo ambayo italeta maendeleo katika sekta ya utalii kupitia uboreshaji wa miundombinu inayotumiwa na watalii, kuvutia wawekezaji watakaokuja  kuwekeza ndani na nje ya hifadhi pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi waishio katika maeneo ya karibu na hifadhi.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Ephraim Mwangomo ambaye ndiye Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Nyerere alieleza utayari wa uzinduzi wa uwanja huo ambao unaenda kuleta faida kubwa kwa Taifa kupitia sekta ya uhifadhi na utalii.




Uwanja huo wa ndege utarahisisha wageni kuifikia hifadhi kwa urahisi na kuongeza idadi ya watalii na safari za ndege, pamoja na kuchangia ongezeko la mapato yatokanayo na utalii.

“Hifadhi inategemea kupokea idadi kubwa ya watalii baada ya kukamilika kwa miradi mbalimbali inayotekelezwa ndani hifadhi. Mathalan, uwanja huu una “Runway” ya urefu wa kilomita 1.8 na utakuwa na uwezo wa kupokea ndege zenye abiria 50 pamoja na ndege ndogo, hali itakayochochea kuongezeka kwa idadi ya watalii na mapato yatokanayo na shughuli za utalii” alieleza Kamishna Mwangomo.

Awali akitoa maelezo, ya mradi huo Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na msimamizi wa mradi huo Mhandisi Michael Joseph alieleza kuwa jengo la abiria la  uwanja huo lina uwezo wa kuhudumia jumla ya wageni 140 wanaoingia (Arrivals) na wageni 140 wanaotoka (Departures) kwa wakati mmoja huku ukiwa na “Control Tower” kwa ajili ya kuongozea ndege, sehemu za maegesho ya magari 90, jengo la kikosi cha Zimamoto na uokoaji, maeneo ya kupumzikia wageni pamoja na ofisi mbalimbali kwa ajili ya uendeshaji wa uwanja.

Miradi mingine iliyokaguliwa ni pamoja na lango la kuingilia watalii la Mtemere, Nyumba za kulala Askari, Nyumba za kualala wageni (Rest House), na Kambi ya kuala watalii (Campsite). Katika ziara hiyo, Dkt. Abbasi iliambatana na viongozi wengine kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.








Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI