Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
WAZIRI wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa [TAMISEMI] Prof. Riziki Shemdoe ametoa miezi sita kwa uongozi wa Mkoa wa Morogoro kuhakikisha unakamilisha ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo ili iweze kutumika na wataalamu wa Ofisi hiyo na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wanachi wa Mkoa huo.
.Prof. Shemdoe alitoa agizo hilo akiwa ziarani mkoani humo na kukagua miradi ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo huku akisisitiza kuwa hakuna haja ya kuendelea na Mkandarasi ambaye hana uwezo wa kumaliza kazi kwa wakati.
Aidha, Waziri huyo aliagiza kutafuta Mkanadarasi mwenye uwezo wa kumalizia ujenzi wa mradi wa jengo hilo huku akitoa wiki moja kuandaa mpango kazi unaotekelezeka wa umalizaiji wa jengo hilo utakaoandaliwa na msitiri, Msimamizi na Mkanadarasi na kuuwasilisha mpango huo katika Ofisi yake.
“Kama Mkandarasi hawezi kazi si atafutwe mtu mwingine wa kumalizia, Sasa mimi nielekeze hivi, kaeni na Client, Consultant na Contractor na baada ya wiki moja mniletee mpango kazi ambao unatekelezeka,”alisema Waziri huyo.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa alisema amepokea maelekezo ya waziri na atayatekeleza huku akitilia shaka uwezo wa mkandarasi anayejenga jengo hilo kama ataendelea na kazi hiyo kwa kuwa amesema ameonesha kuwa na uwezo mdogo katika kutekeleza kazi hiyo.
Mkurugenzi wa Miradi wa Kampuni ya (MCD) ya Chuo Kikuu na Tecknolojia Mbeya ambaye ndiye Mkanadarasi wa ujenzi wa mradi huo Arch Katabaro alikiri kupokea maagizo ya Waziri na kuyatekeleza na kwamba wapo tayari kuendelea na ujenzi huo na kukamilisha ifikipo mwezi Julai mwaka huu kama alivyoagiza.
Pamoja na mradi huo, Waziri alitembelea miradi mingine ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ukiwemo ujenzi wa Barabara ya Kihonda – Veta, Ujenzi wa standi ya Daladala eneo la SGR na Hospitali ya Manispaa iliyopo Mkundi huku akimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Emmanuel Mkongo kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa Hospitali hiyo.
Akiwa katika Halmashauri ya Morogoro DC Waziri Prof. Shemdoe alitembelea Ujenzi wa shule ya Sekondari Ng’aro na kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmadhauri hiyo kutenga fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Maabara ya Shule hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo aliagiza uongozi wa Mkoa huo kuhakikisha maeneo yote ya Taasisi za Serikali pamoja na majengo yake yanapimwa na kupewa hati miliki lakini pia maeneo hayo kuhakikisha yanazungushiwe uzio ili yabaki salama na kuepusha uvamizi.
Mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambao utagharimu shilingi 6.5 Bil. hadi kukamikika kwake, ulianza kutekelezwa mwaka 2022 na kwa mujibu wa mkataba ulitarajiwa kukamilika mwaka 2024 na kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 69 ya utekelezaji wake.
Mwisho..





0 Comments