Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WATUMISHI wa Serikali za Mitaa wametakiwa kuzingatia maadili ya kazi na utumishi wa Umma ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima inayosababisha kushambuliana au kurushiana maneno kati yao na Viongozi wakuu wa Serikali au Wanasiasa.
Wito huo umetolewa Leo Januari 15,2026 na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Deus Sangu, alipokuwa akizungumza jijini Dodoma katika Kikao cha 31 cha Baraza la Taifa la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU).
Amesema kuwa ili kuondokana na migogoro hiyo, kila mtumishi wa Umma anapaswa kuzingatia maadili ya kazi kwa kuepuka vitendo vya uongo, uzembe, pamoja na ubadhirifu wa fedha na mali za umma.
Sangu ameeleza kuwa mikutano ya vyama vya wafanyakazi ni haki ya kikatiba na serikali imekuwa ikishirikiana na vyama hivyo katika kutatua migogoro, ikiwemo kuwatetea watumishi pale wanapotendewa kinyume cha maadili, kama vile kupewa lugha isiyo ya staha au kupewa miradi na kufanya kazi chini ya kiwango kinachotakiwa.
Ameongeza kuwa watumishi wa serikali za mitaa ni mhimili muhimu katika utoaji wa huduma kwa wananchi, huku Rais wa Awamu ya Sita akiendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa kupandisha madaraja, kuajiri watumishi wapya hususan katika sekta ya afya na kuimarisha vyama vya wafanyakazi.
Amesema hata katika kipindi ambacho ajira zilisimama, Rais aliridhia kuendelea kutoa ajira na mchakato huo unaendelea.Aidha, amewatoa hofu watumishi kuhusu suala la mafunzo, akisema serikali itaendelea kutoa fursa za mafunzo kwa watumishi wa umma.
Kuhusu kero ya ucheleweshaji wa malipo ya fedha za likizo, amesema mapendekezo yalishawasilishwa na akabainisha kuwa fedha za malimbikizo ya likizo kwa watumishi wa serikali za mitaa zinapatikana na zitaendelea kulipwa.
Pia Katika suala la miundo ya utumishi, amesema baadhi ya miundo imeanza kurekebishwa baada ya kubainika kuwa baadhi ya watumishi walikuwa wakiongeza elimu bila kunufaika katika ajira zao.
Akisoma risala ya chama hicho, Kaimu Katibu Mkuu wa TALGWU, Komredi Wandiba Ngocho, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kushughulikia kero za watumishi wa umma, hususan upandishwaji wa madaraja, ujenzi wa vituo vya afya, utoaji wa mafunzo pamoja na uboreshaji wa mifumo ya rasilimali watu.
Hata hivyo, amesema changamoto ya kutolipwa kwa wakati fedha za likizo kwa watumishi wa serikali za mitaa bado ni kubwa, akibainisha kuwa baadhi ya watumishi hawajalipwa tangu mwaka 2018 na ameomba serikali kutenga fedha maalum ili kumaliza tatizo hilo ambalo linaendelea kuongezeka kila mwaka.
Ameeleza pia kero nyingine zikiwemo ucheleweshaji wa malipo ya fedha za uhamisho, upungufu wa watumishi wa afya pamoja na wanasiasa kuwanyanyasa au kuwazalilisha watumishi wa umma wanapotekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TALGWU Taifa, Tumaini Yamuhoka, amesema chama hicho si cha migomo bali hupendelea kukaa mezani na kujadiliana, akisisitiza kuwa kwa kiasi kikubwa masuala mengi yanaendelea vizuri.










0 Comments