Matukio Daima, Kilosa
WANANCHI wa kijiji cha Mbuyuni kata ya Rudewa wilayani Kilosa mkoani Morogoro wameeleza wasiwasi wao juu ya mgogoro wa ardhi unaoendelea kati ya wakulima na wafugaji katika eneo la Mtafuteni wakisema hali hiyo imeathiri maandalizi ya msimu wa kilimo ulioanza hivi karibuni.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara wa kijiji wananchi hao wamesema eneo hilo la mashamba ya ukubwa wa zaidi ya hekta 1500 limekuwa na mvutano wa muda mrefu kuhusu mipaka ya matumizi ya ardhi hali iliyosababisha kusitishwa kwa shughuli mbalimbali na Serikali ya wilaya wakati uchunguzi ukiendelea ili kupatikana muafaka.
Wananchi wanadai maeneo hayo wamekuwa wakiyalima kwa muda mrefu lakini kumekuwa na sintofahamu ya mipaka kwa mujibu wa ramani za mgawanyo wa vijiji.
Baadhi ya wananchi akiwemo Torati Buzika,Yusuph Mtalo na Kim Lukeha wamesema kutokuwepo kwa ufafanuzi wa haraka kumeongeza hofu miongoni mwa wakulima wanaotegemea kilimo kama chanzo chao kikuu cha kipato huku wakisisitiza umuhimu wa kupatikana kwa suluhu ya kudumu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Mbuyuni Bw Ayubu Mayumba amesema uongozi wa kijiji umechukua hatua mbalimbali kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi mbalimbali ili kuhakikisha mgogoro huo unapata ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo na kufuata taratibu zilizopo.
Naye Mwenyekiti wa kitongoji cha Makulunge Bi Joyce Matimbwi amesema eneo la Mtafuteni lina historia kubwa katika matumizi ya ardhi hivyo wanaamini haki itatendeka na wananchi kuendelea na Kilimo.
Mkuu wa wilaya ya Kilosa Bw Shaka Hamdu Shaka ameahidi kwenda tena kijijini hapo mapema karibuni ili kuzungumza na wananchi baada ya kukamilisha ripoti iliyokuwa ikiangazia sakata hilo









0 Comments