Header Ads Widget

NIDA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA, UZALENDO KAZINI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu amewataka watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kufanya kazi kwa kufuata Kanuni, Taratibu na Sheria zilizowekwa katika Usajili na Utambuzi wa Watu.

Ameyasema hayo Januari 3, 2025 alipokuwa akifungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa NIDA kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha, Pwani.

“Napenda kuwapongeza kwa utendaji kazi wenu mzuri lakini naomba muendelee kusimamia Kanuni, Taratibu na Sheria za Usajili zilizowekwa kwani NIDA ni taasisi muhimu katika maendeleo ya nchi.” alisema Gugu.

Amesema NIDA inafanya kazi muhimu na yenye maslahi mapana ya nchi. Hivyo, watumishi wanatakiwa kuwa wazalendo na waadilifu katika  kulinda na kutunza taarifa za wananchi ambazo wamepewa dhamana ya kuzitunza.


Amewataka wananchi ambao hawajachukua vitambulisho vyao kufika ofisi za Wilaya za NIDA kuvichukua kwa sababu ni nyaraka muhimu ya utambulisho na Serikali imetumia gharama kubwa kuvizalisha.

Kwa upande mwingine, ameipongeza NIDA kwa kuanzisha Short Code ambayo inawawezesha wananchi kupata mrejesho wa huduma za kitambulisho kwa kutumia simu ya mkononi bila malipo.

Amesema huduma hiyo itawawezesha wananchi hasa wa vijijini kupata fursa ya kujua  taarifa zao na hatua mbalimbali za usajili  wakiwa katika maeneo yao bila ya kufunga safari kuzifikia ofisi za wilaya ambazo zipo mbali na makazi yao.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji amesema mpaka sasa kuna zaidi ya vitambulisho 300,000 ambavyo bado havijachukuliwa  kwenye ofisi za wilaya za NIDA.

‘’Napenda nichukue nafasi hii kuwasisitiza wananchi kuchukua vitambulisho vyao katika ofisi zetu za wilaya kwani Serikali imetumia fedha nyingi kuzalisha vitambulisho hivyo” Alisema Kaji.

Amewataka wananchi ambao taarifa zao zina makosa mbalimbali kutumia fursa ya kibali maalumu cha marekebisho ya taaarifa kurekebisha taarifa zao kwani kibali hicho cha mwaka mmoja kitakapokwisha, hapatakuwa na muda wanyongeza.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI