Zaidi ya miti milioni 42 kupandwa katika maeneo mbalimbali
Ihemi - Iringa,
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amezindua rasmi kampeni ya upandaji wa miti Mkoani Iringa ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kulinda mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha uhifadhi endelevu wa misitu.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika katika eneo la Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Kijiji cha Ihemi kwa ushiriki wa viongozi wa serikali, wadau wa mazingira, taasisi mbalimbali pamoja na wananchi, ambapo zoezi la upandaji wa miti lilianza sambamba na utoaji wa elimu kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na misitu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Kheri James amesema kuwa lengo la uzinduzi ni kuendeleza utamaduni wa kupanda miti na amesisitiza kuwa upandaji wa miti haupaswi kuishia kwenye kampeni pekee, bali uende sambamba na utunzaji wa miti hiyo ili kuhakikisha inakua na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
“Miti inapandwa kwa malengo makubwa yafuatayo kwanza kutunza mazingira lakini pili kutamadunisha umuhimu wa utunzaji wa mazingira lakini tatu ni kupanda miti kimkakati na katika eneo hili la kupanda miti kimkakati tumekusudia kuhamasisha wananchi wetu kupanda miti ya kiuchumi kama miti ya mbao lakini, pia kupanda miti ya matunda kwaajili ya lishe lakini pia tumewahamasisha kupanda miti kwaajili ya dawa kwamba miti pia ni dawa katika jamii yetu” alisema Mhe. Kheri James.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amebainisha kuwa Mkoa wa Iringa una nafasi kubwa ya kuwa kinara wa uhifadhi wa mazingira kutokana na hali yake ya kijiografia na uwepo wa rasilimali misitu, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki katika kupanda miti kwaajili ya kupendezesha mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji.
Mhe. Kheri James pia ametoa wito kwa taasisi za umma na binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na sekta binafsi kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kampeni hii kwa kutoa miche, elimu na rasilimali nyingine muhimu, na amesisitiza kuwa kampeni hii imezinduliwa leo lakini kupitia Vijiji, Kata, Tarafa na Wilaya itaendelea kutekelezwa ili kufikka malengo yaliyotarajiwa.
Hata hivyo ametoa wito kwa TFS kuhakikisha wanagawa miche ikiwemo miti ya matunda katika maeneo ya shule ili kuimalisha mkakati wa lishe na hii itaendelea kuwatamadunisha wananchi kupanda miti ya matunda katika mashule na makazi yao.
Naye Afisa Utalii na Maliasili Mkoa wa Iringa Dkt. Bahati Golyama amesema kuwa kwa mwaka huu 2026 Mkoa wa Iringa umelenga kupanda miti zaidi ya milioni 42 na kampeni hiyo itachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa misitu katika uhifadhi wa vyanzo vya maji, upatikanaji wa maligafi katika viwanda vinavyochakata mazao ya misitu na ustawi wa viumbe hai.
Akipokea maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa, Mhifadhi Misitu wa TFS Wilaya ya Iringa Eutropia Mrema amesema kuwa miche iliyozalishwa ni miche ya matunda, vivuli, urembo na miche kwaajili ya kibiashara kama mbao na nguzo.
Amesema miche hiyo inagawiwa kwa wananchi na TFS imeendelea kualika wadau mbalimbali na wananchi kuchukua miche hiyo na kuhakikisha inapandwa hasa katika kipindo hiki cha mvua nyingi.










0 Comments