Header Ads Widget

DC THOMASI MYINGA ASHIRIKI MIAKA 49 YA CCM KWA KUPANDA MITI ATOA WITO KWA WANANCHI SIKONGE KUPANDA MITI



NA MATUKIO DAIMA MEDIA SIKONGE 

MKUU wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Thomas Myinga, ameungana na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wananchi wa Wilaya ya Sikonge katika maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa chama hicho, yaliyofanyika kwa shughuli ya upandaji miti katika Kata ya Usunga, wilayani humo.

Maadhimisho hayo yalilenga kuhamasisha uhifadhi wa mazingira kwa vitendo, hususan kupitia upandaji miti, kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kushuhudiwa nchini na duniani kwa ujumla. 

Shughuli hiyo ilihusisha viongozi wa chama, watendaji wa serikali, vijana, wanawake na makundi mbalimbali ya wananchi waliokusanyika kwa pamoja kushiriki zoezi la kupanda miti katika maeneo yaliyotengwa.


Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mhe. Myinga alisema kuwa maadhimisho ya miaka 49 ya CCM ni fursa muhimu si tu ya kukumbuka historia ya chama, bali pia ya kuonesha kwa vitendo dhamira ya chama na serikali katika kulinda mazingira na rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. 

Alisema  kuwa upandaji miti ni moja ya njia bora na rahisi ya kukabiliana na changamoto za ukame, mmomonyoko wa ardhi na kupungua kwa vyanzo vya maji.

“Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunalinda mazingira kwa kupanda na kutunza miti katika makazi yetu, mashamba, kando ya vyanzo vya maji na maeneo mengine ya wazi. Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto halisi, na suluhisho lake linaanza na sisi wenyewe,” alisema Mhe. Myinga.

Aidha, aliwahimiza wananchi kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa ipasavyo ili iweze kukua na kutoa manufaa yaliyokusudiwa. 

Mnyinga alieleza kuwa kupanda miti bila kuitunza ni hasara ya rasilimali, hivyo kila mwananchi anapaswa kuwa mlezi wa mti alioupanda. Pia alitoa wito kwa viongozi wa ngazi zote kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.


Kwa upande wao, viongozi wa CCM wilayani Sikonge walisema kuwa maadhimisho ya miaka 49 ya chama yamechagizwa na kaulimbiu ya kuunganisha maendeleo ya kisiasa na kijamii na ulinzi wa mazingira.

 Walieleza kuwa CCM itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhimiza shughuli za maendeleo endelevu zinazozingatia ustawi wa wananchi na mazingira yao.


Wananchi walioshiriki katika zoezi hilo walieleza kufurahishwa na hatua ya kuadhimisha siku hiyo kwa vitendo, wakisema kuwa upandaji miti ni urithi muhimu kwa watoto na vizazi vijavyo. Walisema kuwa wapo tayari kuunga mkono juhudi za serikali kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za utunzaji wa mazingira.

Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa zoezi la upandaji wa miti mbalimbali, ikiwa ni pamoja na miti ya kivuli na matunda, huku viongozi na wananchi wakiahidi kuendelea kushirikiana katika kulinda na kutunza mazingira ya Wilaya ya Sikonge.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI