Na, Chausiku Said
Matukio Daima App Mwanza.
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imesitisha kibali cha udahili na usajili wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika programu ya shahada ya udaktari wa binadamu katika Chuo Kikuu cha afya Cha Mwanza (MzU) kwa mwaka wa masomo 2025/2026.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Desemba 2, 2025 Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, Prof. Charles Kihampa, ameeleza kuwa Tume iliratibu maombi ya udahili kwa vyuo vyote vya elimu ya juu Nchini, ambapo maombi yalitumwa moja kwa moja kwa vyuo vyote hivyo Vyuo viliendelea na utaratibu wa udahili kwa kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu za udahili na uendeshaji wa elimu ya chuo kikuu.
Prof. Kihampa alisema kuwa baada ya kumalizika kwa zoezi la udahili, Tume ilifanya ukaguzi wa awali ili kuona kama vyuo vimezingatia vigezo vya udahili, ikiwemo idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa na usajili wa programu za kitaaluma, hata hivyo, ukaguzi huo ulibaini kuwa Chuo Kikuu cha Mwanza kilifanya ukiukaji mkubwa wa taratibu, ambapo chuo kilidahili idadi kubwa ya wanafunzi mara kumi zaidi ya ile iliyothibitishwa na Tume kwa shahada ya udaktari wa binadamu.
"Tume imebaini kuwa idadi hii ni kubwa kuliko uwezo wa chuo kwa upande wa miundombinu ya kujifunzia, vifaa, na walimu waliopo hii inatishia ubora wa elimu na kuwaweka katika hatari wahitimu wa baadaye," alisema Prof. Kihampa.
Kwa msingi wa ukiukaji huo, Tume imechukua hatua ya kusitisha kibali cha udahili na usajili kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa shahada ya udaktari wa binadamu kwa mwaka wa masomo 2025/2026, na ameeleza kuwa chuo kikuu Cha Mwanza kuwataarifu wanafunzi husika kuwa chuo hicho hakitatoa masomo Kwa Mwaka wa kwanza katika Mwaka wa masomo 2025/2026.
Aidha ameeleza kuwa Katika kikao maalum cha Tume kilichofanyika tarehe 28 Novemba 2025, Tume ilifanya maamuzi na kukitaka Chuo Kikuu cha Mwanza kuepuka kuendelea na udahili wa idadi kubwa ya wanafunzi kuliko ile inayoruhusiwa. Hata hivyo, wanafunzi waliodahiliwa kwa mwaka huu wataruhusiwa kuhamia vyuo vingine vinavyoruhusiwa kudahili program ya udaktari wa binadamu.
Pia, Tume imeagiza kwamba wanafunzi wote walioathirika na mabadiliko haya watapewe fursa ya kuhamia vyuo vingine vilivyoruhusiwa, au kuchagua programu nyingine za masomo kwa mwaka wa masomo 2025/2026 au miaka inayofuata.
"Chuo Kikuu cha Mwanza kimeelekezwa kuhakikisha kinawasaidia wanafunzi hao kutafuta vyuo vingine na pia kimeambiwa kutowapeleka wanafunzi hao kwa masomo yoyote ya mwaka huu wa masomo. Hii ni kwa sababu chuo hicho hakikidhi vigezo vya udahili na miundombinu kwa sasa," alisema Katibu Mtendaji.
Tume pia imetangaza kuwa itashirikiana na Chuo Kikuu cha Mwanza pamoja na vyuo vitakavyowapokea wanafunzi kuharakisha mchakato wa uhamisho wa wanafunzi, ili kuhakikisha hakuna madhara kwa elimu ya wanafunzi.
Hata hivyo,Tume imetangaza kuwa itaunda timu ya wataalamu kuchunguza masuala ya kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Mwanza, ili kuchukua hatua stahiki za kurekebisha hali hiyo na kuhakikisha kuwa chuo kinazingatia sheria na taratibu zinazotawala elimu ya chuo kikuu.
Kamati hiyo ya wataalamu itaanza kazi mara tu baada ya zoezi la uhamisho kukamilika.









0 Comments