Header Ads Widget

TAWA YAKABIDHI BWENI LA WASICHANA SHULE YA SEKONDARI MCHENGERWA, RUFIJI


Na Beatus Maganja, Rufiji, Pwani.

 MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imekabidhi rasmi bweni jipya la wasichana katika Shule ya Sekondari Mchengerwa iliyopo Kata ya Ngarambe wilayani Rufiji mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya elimu, hasa kwa mtoto wa kike.

Bweni hilo ambalo ujenzi wake umegharimu zaidi ya shilingi milioni 252, limejengwa kwa ushirikiano kati ya TAWA na Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori  (Frankfurt Zoological Society – FZS) chini ya ufadhili wa Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya watu wa Ujerumani (KfW), limekabidhiwa likiwa na jumla ya vitanda 40 aina ya "double decker", magodoro 80, huduma ya maji safi, pamoja na umeme unaohudumia wanafunzi wapatao 80.

Mbali na bweni hilo, TAWA pia imekabidhi darasa moja la kisasa likiwa na meza 45 na viti 45 vya wanafunzi pamoja na viti vinne na meza mbili za walimu katika shule ya Sekondari Mwaseni wilayani humo, vyote vikiwa na thamani ya shillingi millioni 60 na kufanya miradi yote miwili iliyokabidhiwa kuwa na thamani ya zaidi ya shillingi millioni 312




Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano na uzinduzi wa miradi iliyofanyika wilayani humo Disemba 03, 2025, Mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Abraham Jullu alisema ujenzi wa mradi huo uliotokana na mradi wa dharura wa kupambana na majanga ya UVIKO - 19 (ERB) unalenga kuondoa changamoto ya mazingira duni ya kujisomea na kujifunzia  kwa wanafunzi hususani wanafunzi wa kike ambao wamekuwa wakitembea umbali mrefu kwenda shuleni na hivyo kuwa hatarini dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu.

 “TAWA inaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wa maendeleo kuhakikisha jamii zinazozunguka maeneo yetu ya hifadhi zinapata huduma bora za kijamii. Uwekezaji huu katika elimu ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu wetu wa kijamii kupitia shughuli za uhifadhi, kujenga mahusiano mazuri na jamii ili kuhakikisha, usalama, utulivu na ustawi wao katika nyanja mbalimbali” alisema.

"Bweni hili litaboresha kwa namna kubwa mazingira ya masomo Kwa wanafunzi wa kike, litawaweka mahali salama, Karibu na shule na litawapa muda zaidi wa kujisomea na kupumzika bila hofu ya wanyama hatari wala safari ndefu. Hii ni hatua muhimu katika kuongeza ufaulu, usawa na fursa za elimu na kulinda haki ya mtoto wa kike kupata mazingira bora ya kujifunzia" aliongeza

Naye Mkurugenzi Mkaazi wa FZS Dkt. Maurus Msuha alisema shirika hilo litaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika suala la uhifadhi na kushirikiana katika kuboresha huduma za elimu kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha. Aidha alibainisha kuwa uwekezaji katika elimu ya mtoto wa kike ni msingi wa maendeleo ya jamii.









Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji  Mhe. Luteni Kanali Fredrick Komba aliishukuru TAWA  na wadau wake kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kutatua changamoto mbalimbali za kijamii hususani katika kuboresha sekta ya elimu wilayani humo sambasamba na kudumisha mahusiano mazuri na jamii zinazozunguka Hifadhi ya Selous.

Vilevile aliipongeza Serikali ya Ujerumani Kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kufanikisha masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kimaendeleo.

“Hatua hii itasaidia kuongeza ufaulu, kuboresha nidhamu na kupunguza utoro miongoni mwa wanafunzi wa kike. Tunaishukuru TAWA, FZS na Serikali ya Ujerumani kwa kuona umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya watoto wetu,” alisema Luteni Kanali Fredrick Komba 

Wazazi, walimu, wanafunzi na viongozi wa vijiji vya Ngarambe na Mwaseni walipongeza juhudi hizo wakisema ujenzi wa miradi hiyo ni uthibitisho wa dhahiri kuwa TAWA haitumii tu rasilimali za taifa Kwa ajili ya uhifadhi, bali inarejesha sehemu ya faida hizo Kwa jamii zinazowazunguka

Aidha wamesema miradi hiyo imekuwa faraja kubwa kwa wanafunzi wa kike ambao hapo awali walikabiliwa na changamoto ya kutembea masafa marefu, usalama na mazingira duni ya kujisomea pia ujenzi wa darasa utapunguza msongamano mkubwa wa wanafunzi darasani.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI