Na Ashrack Miraji Matukio Daima App
Serikali inatarajia kununua ndege mpya nane kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), hatua itakayoongeza uwezo wa shirika hilo kupanua safari zake za ndani na nje ya nchi. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema pamoja na ongezeko hilo, ni muhimu ATCL kupunguza gharama za uendeshaji na kuhakikisha tija inaongezeka.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kwanza cha Baraza la Wafanyakazi wa ATCL kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Profesa Mbarawa alisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia, kuondoa safari zisizo na faida, na kuhakikisha ndege zinatumika kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Mhandisi Peter Ulanga, alisema ujio wa ndege hizo utaimarisha huduma za shirika, kuongeza ushindani na kupanua mtandao wa safari za kitaifa na kimataifa. Ameeleza kuwa mwongozo madhubuti kutoka Wizara ya Uchukuzi umeendelea kuwezesha shirika hilo kukuwa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Profesa Neema Mori, amepongeza kufanyika kwa kikao hicho na kusisitiza kuwa Bodi itaendelea kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ili kuimarisha utendaji, ushindani na ufanisi wa shirika.
Kikao hicho kimewakutanisha menejimenti na wawakilishi wa wafanyakazi kujadili masuala muhimu yanayohusu uendeshaji, ustawi wa wafanyakazi, uboreshaji wa huduma na mikakati ya kuongeza ufanisi wa shirika.











0 Comments