Header Ads Widget

RC MALIMA AAGIZA MRADI WA ECO SCHOOL USAMBAZWE WILAYA ZOTE MOROGORO

 

Na Lilian Kasenene,Kilosa

Matukio DaimaApp 

MKUU wa mkoa wa Morogoro Adam Malima ameagiza mradi wa utunzaji mazingira(ECO SCHOOLS) kwa taasisi za elimu usambazwe katika wilaya zote za mkoa huu. 

Alisema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi bendera za kijani na vyeti kwa shule zinazotekeleza mradi huo kwa mikoa ya Morogoro na Iringa.


"Mradi huu unatekelezwa kwa wakati muafaka kwani ndio kipindi cha utekelezaji wa Mtaala mpya wa elimu,"alisema Malima.


Katika hotuba yake iliyosomwa na mkuu wa wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka, Malima alisema utunzaji wa mazingira unapaswa kufundishwa kwa watoto wa ngazi zote za shuleni.


"Utunzaji wa mazingira uwe sahemu ya malezi kwa watoto wa ngazi zote ukiwa na mbinu shirikishi kwa jamii nzima," alisema mkuu huyo wa mkoa.



Mkurugenzi wa shirika la kuhifadhi misitu asili Tanzania (TFCG) Charles Meshack akizungumza wakati wa hafla hiyo,alisema hadi sasa mradi wa ECO SCHOOLS unaendeshwa katika shule 200 zilizopo kwenye mikoa  ya Morogoro, Tanga, Iringa, Lindi na Mtwara.


Alisema mradi huo wa ECO SCHOOLS pamoja na kutunza mazingira unasaidia watoto kujifunza kwa vitengo yale wanayofundishwa darasani.

"Mradi wa ECO SCHOOLS umeanza kuigwa na jamii zinazozunguka shule kwani miradi hiyo inasaidia katika kujiingizia kipato na hata shule zenyewe zimejianzishia miradi midogo,"alisema Meshack.


Mkurugenzi huyo ambaye ndiye meneja mradi wa ECO SCHOOLS Tanzania alisema jumla ya shule 41 zimepata bendera ya kijani na shule tano zimepata vyeti baada ya kukidhi vigezo saba vilivyohitajika katika utunzaji wa mazingira.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Dumila ambayo ni kati ya waliopokea bendera ya kijani Faraja Tematema alisema mradi wa ECO SCHOOLS umechangia kuongeza ufaulu mzuri na kupunguza utoro wa wanafunzi

 

Tematema alisema pia ECO SCHOOLS imesaidia kuongezeka kwa uelewa umuhimu wa utunzaji mazingira kwa watoto kwa kujifunza kwa vitendo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI