Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
MASHINDANO ya Shirikisho la Michezo ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) yaendelea kutimua vumbi mkoani Morogoro katika viwanja mbalimbali mjini Morogoro.
Chuo Taifa cha Usafirishaji (NIT) ni miongoni mwa Taaisi zinazoshiriki mashindano hayo, awamu hii ikitinga na wachezaji 62 kushiriki michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, pete, wavu, volleyball, riadha na michezo ya jadi.
Mkuu wa Chuo cha NIT Prof. Prosper Mgaya, alisema washiriki wa timu zote za chuo hicho wameendelea kufanya vyema kwa michezo waliyoshuka dimbani, katika hatua za makusudi wapo nafasi ya kwanza na ya pili kwa baadhi ya michezo, hatua inayotoa taswira ya timu hizo kufuzu hiyo.
"Sasa toka tumeanza kushiriki mashindano haya tumeshiriki mchezo wa mpira wa miguu, pete, kamba, volleyball na mingine ya jadi, ninafurahi sababu washiriki wetu mpaka sasa wanafanya vizuri, ukiangalia hata hatua ya makundi wamefanya vizuri,"alisema Prof. Mgaya
Kwa upande wake Mkufunzi wa Michezo NIT Sigfrid Msaghaa alisema ushiriki wa wanamichezo katika taasisi yao umeongezeka ikilinganishwa na idadi ya walioshiriki michezo ya mwaka 2024 iliyofanyika mkoani Tanga ambapo walishiriki wachezaji 18 pekee na walishiriki michezo miwili tu mpira wa miguu na Volleyball.
Alisema ongezeko la washiriki ndilo linabeba tumaini la wao kufanya vyema zaidi katika mashindano hayo, na kwamba jukumu lao kubwa ni kuhakikisha wanang'arisha jina la chuo hicho.
Naye Nahodha wa Timu NIT kwa mchezo wa Mpira wa Miguu Victor Mbezi alisema katika kundi lao linajumuisha michezo saba katika hatua ya awali ya makundi, ambapo wameshuka dimbani kwa michezo mitano, wakishinda michezo miwili, wakitoa suluhu michezo na wakipoteza mchezo mmoja.
Alisema hadi sasa katika kundi lao kwa mchezo wana nafasi ya kufuzu hatua ya makundi, akidhatiti kwa ubora wa kikosi chao anaamini watasonga mbele katika mashindano hayo.
...









0 Comments