Header Ads Widget

JMAT YATOA ONYO KWA VIONGOZI WA DINI, YAPENDEKEZA MAOMBI YA TAIFA KUREJESHA AMANI

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

JUMUIYA ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) imetoa tamko kali kwa baadhi ya viongozi wa dini wanaotoa kauli zinazodai kuwepo kwa mpasuko wa kidini kati ya Waislamu na Wakristo, ikisisitiza kuwa jamii inapaswa kulinda misingi ya amani na maridhiano.

 Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Alhad Mussa Salumu amesema JMAT imeweka wazi msimamo wake kuhusu mfululizo wa matamko makali yaliyotolewa siku za karibuni, akibainisha kwamba lugha za uchochezi kutoka kwa viongozi wa dini zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa ustawi wa taifa.

Alhad Salumu amesema jumuiya hiyo inapendekeza kufanyika kwa maombi ya kitaifa yatakayounganishwa na mfungo wa siku tatu kwa Waislamu na Wakristo katika mikoa na wilaya zote nchini, lengo likiwa kuombea amani, kuponya majeraha ya kijamii na kujenga maridhiano ya kudumu.

 Ameeleza kuwa vurugu za Oktoba 29, 2025 wakati wa Uchaguzi Mkuu zilisababisha vifo vya vijana 14, kupotea kwa mali za wananchi, athari za kisaikolojia na mtikisiko wa kiuchumi, hali iliyosababisha ongezeko la chuki na mashaka baina ya watu wa dini tofauti.

Amesema pia kuwa JMAT inataka uchunguzi kamili ufanyike ili kubaini chanzo cha vurugu hizo na kutoa suluhisho la kudumu.

 Aidha, jumuiya hiyo imeomba kukutana na Rais ili kujadiliana kuhusu hatua za kitaifa za kudumisha umoja, huku ikisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili kuepusha kusambaa kwa taarifa za uchochezi.

Vijana ndio walioathirika zaidi katika vurugu hizo, baadhi yao walichochewa na wanaharakati wa ndani na nje ya nchi, huku mitandao ya kijamii ikitumika kusukuma ajenda potofu, " Amesema
Alhad Salumu 

Katika tamko hilo, JMAT ilimpongeza Rais kwa kulifungua Kanisa la Ufufuo na Uzima na kumshukuru Waziri Mkuu kwa jitihada za kurejesha amani nchini.

Aidha, jumuiya imetaka serikali kuimarisha udhibiti wa wageni wanaoingia nchini, ikisema kuna madai kwamba baadhi yao walihusika kwenye machafuko ya Oktoba 29.

Kwa upande wake, Mama Terry ambaye ni mwanaharakati wa amani, amesisitiza umuhimu wa kuwasikiliza vijana na kuunda majukwaa mahususi ya mazungumzo ili kuzuia mazingira ya hofu na ukatili. 

"Vjana wana machungu makubwa na kwamba hakuna uchungu mkubwa kama mzazi kumzika mwanae hivyo jamii ni lazima ishirikiane katika kuwajenga upya kisaikolojia, " Amesema.

 Mama Terry alionya pia dhidi ya tabia ya watu kuteswa au kutekwa kwa kuuliza maswali au kutoa maoni, akisema taifa linahitaji uhuru wa kujieleza bila vitisho.

Naye Mchungaji Kuani Mussa aliitaka jamii kuiweka amani mbele kila wakati, akisisitiza kwamba mafanikio ya nchi hayawezi kupatikana bila utulivu.

Amesema taasisi za dini zinapaswa kutoa elimu ya amani na msamaha ili kuondoa chuki iliyojengeka kufuatia matukio ya hivi karibuni.

JMAT imesisitiza kwamba jukumu la kurejesha amani na kuponya taifa ni la kila mmoja, na kwamba maombi, maridhiano na mazungumzo ya wazi ndio njia pekee ya kuondoa msuguano uliopo na kujenga msingi imara wa umoja wa kitaifa.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI