Header Ads Widget

DODOMA YAPAZA SAUTI: WANANCHI WAOMBA ZOO KUBADILI USO WA UTALII NA ELIMU YA VIZAZI VIJAYO

 


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

WANANCHI wa Mkoa wa Dodoma wameiomba Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuanzisha bustani ya wanyama (Zoo) katika mkoa huo ili kuongeza vivutio vya utalii wa ndani na kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wamesema uanzishwaji wa bustani ya wanyama utakuwa hatua muhimu katika kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha utalii wa ndani, ikizingatiwa kuwa mkoa huo ni makao makuu ya nchi na unatembelewa na watu wengi kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Wamebainisha kuwa uwepo wa bustani ya aina hiyo utasaidia kuongeza fursa za ajira, kukuza biashara ndogo ndogo, pamoja na kutoa elimu kwa wanafunzi na vijana kuhusu uhifadhi wa wanyama na mazingira.

Aidha, wananchi wameitaka TAWA kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, Serikali za Mitaa na sekta binafsi ili kuhakikisha mpango huo unafanikiwa kwa wakati na kuleta manufaa kwa jamii.

Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa maeneo mbalimbali ya Dodoma wametoa wito kwa Serikali kutazama kwa karibu pendekezo hilo, wakisisitiza kuwa bustani ya wanyama itaimarisha hadhi ya jiji na kuongeza mapato ya utalii nchini.

Mwenyekiti mstaafu wa Mtaa wa Uhindini Dodoma, Alnoor Kassam Visram, amesema kuwa ujenzi wa eneo maalumu la hifadhi ya wanyama (Zoo) unaweza kuwa fursa muhimu kwa jamii ya mtaa huo endapo utasimamiwa kwa umakini na kuzingatia usalama wa wakazi.

Amesema zoo inaweza kuwa kivutio cha utalii, kutoa ajira kwa vijana na kuwa sehemu ya elimu kwa watoto kuhusu uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa mamlaka husika kuhakikisha miundombinu inajengwa kwa viwango pamoja na kuweka mifumo madhubuti ya usimamizi ili kuepusha changamoto kama harufu, kelele au kutoroka kwa wanyama ambayo inaweza kuathiri amani ya wakazi.

Daniel Mkate, mkazi wa Mlezi Dodoma, amesema Dodoma sasa ni makao makuu ya nchi na miongoni mwa miji inayokua kwa kasi kubwa nchini Tanzania.

Amesema pamoja na kuwa na maeneo mengi ya wazi, mji huo umeendelea kuvutia watu kutoka sehemu mbalimbali, hasa wakati wa vikao vya Bunge, mikutano ya kisiasa na shughuli nyingine za kitaifa

Tangu mwaka 2016, baada ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kutangaza rasmi kuhamia Dodoma kwa Serikali Kuu, kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaohamia mjini hapo kwa ajili ya makazi na kazi.

Amesema wageni wengi wanatokea Jiji la Dar es Salaam ambako kuna huduma mbalimbali ikiwemo mabustani ya wanyama (Zoo) ambayo watoto hutembelea mara kwa mara kuona wanyama kama simba, tembo na wengine.

“Kwa sasa Dodoma haina zoo, hali inayosababisha kukosekana kwa fursa muhimu ya mapato kwa mkoa pamoja na kukosa huduma za burudani na mafunzo kwa vitendo kwa watoto,” amesema.

Ameongeza kuwa wakati wa sikukuu na mapumziko ya kitaifa watoto wengi hukosa mahali pa kujifunza na hubaki kupiga picha kwenye maeneo kama Nyerere Square.

Ameeleza kwamba uwepo wa zoo unaweza kuwasaidia watoto kusoma kwa vitendo, kuona wanyama halisi na kuongeza hamasa ya ujifunzaji.

“Zaidi ya hayo, zoo inaweza kuongeza utalii wa ndani kama ilivyo katika miji mingine kama Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Tabora,” amesema.

Ameongeza kuwa si lazima Serikali pekee ihusike, bali hata watu binafsi au wawekezaji wana uwezo wa kuanzisha zoo Dodoma, jambo ambalo litatoa ajira, kuongeza mapato na kuifanya Dodoma kuwa mji wenye vivutio zaidi.

Naye Prisca Philemon, mkazi wa Nzuguni Dodoma, amesema kuwa mji huo unakua kwa kasi na kuvutia watu kutoka sehemu mbalimbali za nchi.

Amesema Dodoma sasa ni kitovu cha shughuli nyingi za Serikali na mikutano ya kitaifa, lakini bado inakosa jambo moja la msingi zoo ya kuwapa watoto fursa ya kujifunza na kuburudika.


Amesema licha ya maendeleo yote, mji huo hauna mahali pa kutazama wanyama kwa karibu kama ilivyo katika miji mingine.

Katika nyakati za sikukuu na mapumziko, wazazi wengi hukosa sehemu ya kuwapeleka watoto zaidi ya viwanja vya wazi kama Nyerere Square.

“Watoto wanatamani kuona wanyama halisi, na mara nyingi tunabaki kuwaambia tu, ‘Wakifika Dar es Salaam watawaona hili linatuumiza kama wazazi maana elimu kwa vitendo ni muhimu sana katika makuzi ya mtoto,” amesema.

Ameeleza kuwa uwepo wa zoo Dodoma ungeongeza utalii wa ndani na kuleta mapato kwa mkoa.

Amesema watu wengi wanaokuja kwa shughuli za Bunge, mikutano au kazi mbalimbali wangependa kuwa na sehemu ya kutembelea wakati wa mapumziko.

Ameongeza kuwa Dodoma ina nafasi, ina watu na ina soko kinachokosekana ni uwekezaji tu.

Amesema wawekezaji binafsi wana uwezo mkubwa wa kuanzisha zoo kama ilivyo katika miji ya Arusha, Mbeya na Dar es Salaam.

“Hii si tu kwa ajili ya burudani, bali kwa ustawi wa watoto wetu, elimu yao na hadhi ya mji wetu kama makao makuu ya nchi kuwepo kwa zoo Dodoma kutakuwa sio tu kivutio cha utalii, bali pia urithi wa vizazi vijavyo,” amesema.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI