Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam, Disemba 03, 2025.
Serikali imeipongeza Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa kuendelea kuwa chimbuko la wataalamu na wabunifu wanaojibu mahitaji halisi ya jamii, huku ikitangaza mpango mpya wa kitaifa wa kuelekeza maendeleo ya teknolojia nchini kwa miongo ijayo.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Ladslaus Laurent MnyoneMkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika wizara hiyo amesema hafla ya kutunuku wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma na kwenye ubunifu ni “ishara tosha kuwa Tanzania ina rasilimali watu yenye uwezo wa kulipeleka taifa kwenye uchumi unaotegemea teknolojia.”
Katika hotuba yake, Mkurugenzi huyo amesema Serikali iko katika hatua za mwisho kuandaa "National Technology Roadmap" mkakati wa kitaifa utakaoainisha mahitaji ya kiteknolojia ya nchi kwa kipindi cha miaka 20 hadi 30 ijayo katika sekta mbalimbali.“Tunahitaji teknolojia inayotatua changamoto zetu, sio teknolojia ya kuiga. Roadmap hii itawaongoza vijana wetu na taasisi kama DIT kutengeneza bunifu zinazojibu mahitaji ya nchi,” amesema.
Ameeleza kuwa mpango huo utafungua fursa nyingi za uwekezaji, kuongeza ajira na kusaidia watafiti kuelekeza nguvu kwenye maeneo yenye tija kubwa kitaifa.
Mkurugenzi huyo amesema amefarijika kuona idadi kubwa ya wanawake miongoni mwa wanaotunukiwa tuzo na zawadi.
“Hii ni dalili njema kwa Taifa. Wanawake na wasichana wako karibu sana na uhalisia wa maisha yetu. Wakiwa wabunifu na wahandisi, ubunifu wao utaakisi mazingira yetu,” amesema.
Katika salamu zake kwa wadau, amesema kuwa tayari baadhi ya mashirika makubwa ya Serikali kama Shirika la Reli (TRC) yametangaza fursa za ajira kwa wahitimu wa masuala ya teknolojia, akitoa rai kwa sekta nyingine kufuata mkondo huo:
“Tunahitaji mazingira rafiki zaidi ya ajira na kujiajiri. Vijana hawa wakipata ushirikiano, watakuwa sehemu ya mapinduzi ya kiteknolojia nchini.”
Prof. Mnyone Amezitaka taasisi zilizo na vituo vya umahiri—ikiwemo DIT kupitia teknolojia ya ngozi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(ICT) kujitokeza zaidi kwenye hafla kama hizi ili kutambua wanafunzi wenye uwezo wa kipekee na kuwalea kwa ajili ya mafanikio ya kitaifa.
Aidha amehimiza ununuzi wa teknolojia za ndani ili kuwainua vijana wabunifu wakitanzania akibainisha kuwa Tanzania bado inatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza bidhaa za kiteknolojia kutoka nje.“Ni muhimu kama taifa kuwa wanunuzi wakubwa wa teknolojia zinazobuniwa na vijana wetu. Tukishindwa kuzitumia, wabunifu watachoka na watahama kwenye ubunifu. Serikali inapigania hili linatekelezeka.”
Ameongeza kuwa nchi zilizoendelea kama China hupata hadi USD trilioni 1.8 kwa mwaka kupitia mauzo ya bidhaa za teknolojia—akisisitiza kuwa Tanzania ina uwezo wa kuongeza mauzo yake na kupunguza uagizaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa DIT, Prof. Preksedis Marco Ndomba, amewaasa wanafunzi na wahitimu, kuacha kutegemea vyeti vyenye ufaulu wa daraja la juu kama kigezo kikuu cha mafanikio.
“Degree peke yake haitoshi, na ubunifu pekee hautoshi kama hauwezi kuingia sokoni. Unapaswa kuwa industrialist, entrepreneur, mtu wa kazi. Watu hawataki first class yako — wanataka huduma yako,” alisema kwa msisitizo.Prof. Ndomba amebainisha kuwa changamoto kuu kwa vijana si ukosefu wa mtaji kama wengi wanavyodhani, bali ni ukosefu wa uwezo wa kuitangaza na kuiuza taaluma yao kwa wadau.
Ametoa mfano wa watu wasiokuwa na degree za juu lakini wanaongoza viwanda, kampuni za teknolojia na miradi mikubwa kutokana na ujasiri, ubunifu na weledi.
“Msitangaze sana degree yenu — tangazeni ubunifu, ujuzi na huduma. Unyenyekevu, kujituma na uwezo wa kufanya kazi na wadau ndizo silaha za mafanikio,” alisema.
Ameongeza kuwa DIT imefanya kazi kubwa kuzalisha wataalamu wanaojibu changamoto halisi, hasa kwa kuwapeleka wanafunzi katika mazingira ya kazi kabla ya kuanzisha bunifu zao.
Nao wanafunzi na wahitimu waliotunukiwa vyeti na zawadi wameshukuru uongozi wa DIT na waratibu wa zawadi hizo huku wakiahidi kutumia motisha hiyo kuendeleza bunifu zao ili kuleta majawabu ya kiteknolijia katika jamii ya Tanzania.




























0 Comments