Header Ads Widget

BONANZA LA MPIRA WA MIGUU LAZIDISHA MSHIKAMANO WA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA JIJINI MBEYA

 

Na Samwel Mpogole - Mbeya 

Bonanza la mpira wa miguu kwa wanawake lililofanyika jijini Mbeya limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, huku wadau mbalimbali wa maendeleo wakitoa wito kwa jamii kuungana katika kutetea haki na ustawi wa wanawake na wasichana.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa Ustawi wa Jamii wa Jiji la Mbeya ameishukuru jumuiya na mashirika yaliyoshiriki kufanikisha bonanza hilo, akisisitiza kuwa ni muhimu wanawake na wasichana kutoa taarifa mapema pindi wanapokumbana na aina yoyote ya ukatili ili kupata msaada stahiki. Ameeleza kuwa jamii inapaswa kuongeza ushirikiano katika kuzuia na kupambana na ukatili huo, ambao umekuwa ukihatarisha mustakabali wa kundi hilo muhimu.
Kwa upande wake, INSPECTOR Canisio Benard, OCS Msaidizi wa Kituo cha Polisi Mwanjelwa kata ya Iyela, amewapongeza washiriki kwa kujitokeza kwa wingi na kuonesha ari ya kupinga ukatili wa kijinsia. Amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha jitihada za kushirikiana na wananchi katika kutokomeza vitendo vya ukatili, hasa vinavyowalenga wanawake na wasichana.

Akiwakilisha wadau wa uandaaji wa bonanza hilo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Luka Creative, Musa Sango, amesema dhamira kuu ya bonanza ni kutoa hamasa, elimu na kuibua vipaji miongoni mwa wanawake, sambamba na kuongeza mwamko katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia. Amebainisha changamoto kama ukosefu wa taarifa sahihi na hofu ya kuripoti matukio ya ukatili, ambazo kwa mujibu wake zinahitaji nguvu ya pamoja ili kuzitatua.

Shirika la Caritas Based Rehabilitation nalo limetoa wito kwa jamii kuhakikisha watoto wenye ulemavu hawafichwi majumbani, bali wanapewa nafasi ya kupata elimu na huduma zinazowastahili, ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.

Katika mchango wake, mwakilishi wa shirika la COMSOR, Alexandria, amelishukuru Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya kwa ushirikiano wao katika kutoa huduma za ushauri nasaha na ulinzi kwa makundi maalum, akisisitiza kwamba jitihada za pamoja ndizo msingi wa kupunguza ukatili katika jamii.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa bonanza hilo, Helieth Maiko Mkondya ameahidi kuwa balozi madhubuti wa kupinga ukatili katika maeneo yao, huku akiahidi kutoa elimu kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia kwa wasichana na wanawake.

Bonanza hilo limeendelea kuthibitisha kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuunganisha jamii, kujenga uelewa, na kutoa nafasi kwa wanawake kujifunza, kushirikiana na kuinua sauti ya pamoja katika mapambano ya kulinda haki na usalama wa msichana na mwanamke.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI