Diwani wa kata ya Nsalaga jimbo la Uyole Mkoani Mbeya Clemence Mwandemba, amefanya kikao chake cha kwanza na wajumbe wa Baraza la maendeleo ya kata (WDC) akikabidhiwa rasmi ofisi na afisa mtendaji wa kata hiyo.
Katika kikao hicho cha kujitambulisha, Mheshimiwa Mwandemba ameahidi kuhakikisha anawatumikia wananchi bila kuchoka kuhakikisha wanasikilizwa na kero zao zinatafutiwa ufumbuzi.
Pia ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa kutoa mabillion ya fedha kwa ajili ya kata ya Nsalaga ikiwemo ujenzi wa ba barabara za lami na za vifusi, ujenzi wa shule mpya, uboreshaji miundombinu ya maji, umeme na maeneo mengine mbalimbali.
Amesema baadhi ya kero ambazo ni miongoni mwa agenda zake na tayari zimeanza kufanyiwa kazi ni pamoja na uboreshaji miundombinu ya barabara pamoja na vivuko na madaraja yake, umeme kuwafikia wananchi wote kutokana na kata hiyo kuendelea kukua kila uchao na kuendelea kuboresha sekta ya elimu.
Pamoja na hayo amewashukuru watumishi wote wa kata ya Nsalaga na ntangulizi wake Mchungaji David Ngogo (aliyekuwa Mhe. Diwani wa Nsalaga 2020-2025) na wananchi kwa ujumla wao kwa ushirikiano katika kufanikisha miradi ya maendeleo.
Amewaomba kuendelea kushirikiana huku akiwaagiza viongozi wa chini yake katani humo kuhakikisha wanazifanya ofisi za umma kuwa kimbilio la wananchi kwa kuwatumikia kwa uadilifu na nidhamu huku akisisitiza wataalam kubaki kwenye eneo lao na viongozi wa kisiasa kubaki maeneo yao.
Kwa upande wake afisa mtendaji wa kata ya Nsalaga Uyole Joyce Gwega, amesisitiza kila mtaalam kukaa kwenye eneo lake kufanya kazi kama anavyotakikana kwa mujibu wa sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma ili kuwatumikia wananchi na kufikia maendeleo endelevu.
Viongozi mbalimbali wa katani humo ambao ni wajumbe wa kikao hicho wameahidi ushirikiano miongoni mwao na wananchi ili kuhakikisha maendeleo zaidi yanafikiwa.
0 Comments