Wafugaji wa Kata ya Chanika, Wilayani Ilala Mkoani Dar Es Salaam wameishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa mapinduzi na ujio wa miradi mikubwa ya ufugaji iliyowasaidia kujikwamua na umaskini na kuongeza kipato.
Kwaniaba ya wafugaji hao, Bw. Hamim Idrisa, Katibu wa Wafugaji Kata ya Chanika, ameeleza kuwa ipo miradi mitatu iliyozinduliwa katika Kata ya Chanika katika kipindi cha miaka minne ya awamu ya kwanza ya Rais Samia, ambayo imewaneemesha wafugaji ikiwemo mradi wa kuku wa Mayai na mradi wa kukabiliana na usugu wa madawa ya mifugo.
"Mradi wa kwanza ni ufugaji wa kuku bila dawa ambao umekuwa msaada mkubwa sana kwetu, upo pia mradi wa kukabiliana na usugu wa madawa dhidi ya vimelea vya magonjwa na mradi wa mwisho ni huu wa kuku wa mayai ambapo serikali inatupa nyenzo, madawa na elimu kupitia Maafisa tulionao kwenye Kata yetu." Amesema Bw. Idrisa.
Katika upande wa maendeleo ya Jamii na ustawi, Bw. Idrisa amezungumzia sekta ya afya, akiishukuru serikali kwa ujenzi wa Chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Nguvu Kazi pamoja na kuanza kwa mradi wa Zahanati ya Kidugilo, ambapo fedha na eneo la utekelezaji wa mradi huo imeshapatikana.






0 Comments