Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Dodoma
ASKOFU wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika(DCT) Dkt Dickson Chilongani ametoa tahadhari na wito kwa viongozi wa makanisa na waumini wote kushiriki katika maombi ya kuombea amani Taifa.
Akizungumza katika ibada iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu Dodoma,amesema kuna dalili zinazoashiria kutokea kwa misukosuko iwapo uamuzi wa baadhi ya makundi kuandamana utaendelea, hivyo ni wakati wa kanisa kusimama kama ngao ya upatanisho.
"Nadhani mmesikia na baadhi yenu mmeona kwenye mitandao kuhusu tishio la watu kuandamana tena tarehe 9 Desemba. Tusingependa yale yaliyotokea hivi karibuni yajirudie tena," amesema Askofu Chilongani.
Amesema kuwa tukio lolote linalohatarisha usalama, mali na maisha ya watu halina tija kwa taifa, na hivyo suluhisho kuu ni kuombea hali ya utulivu na kuhimiza jamii kuchagua maridhiano badala ya migongano.
Dkt Chilongani amesema kanisa lina wajibu wa kusimama mstari wa mbele katika usuluhishi wa hali za kijamii, kiroho na kitaifa.
Ameagiza kuwa mahubiri ya yahusishe kwa upana mada ya amani na utakatifu, akibainisha kuwa wakristo wanapaswa kuwa mfano unaoonekana katika jamii.
"Mtume Paulo anatukumbusha katika Waebrania 12:14 kwamba amani na utakatifu vinakwenda sambamba," amesema huku akinukuu maandiko matakatifu.
Aidha, Askofu Chilongani ametoa mwelekeo wa kitheolojia kwa waumini akiwahimiza kutekeleza vitu vinne muhimu vinavyoweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii ambavyo ni kufikiri amani, kuomba amani, kuongea amani na kutenda amani.
"Tukifanya hivyo kwenye parishi zetu 300 na makanisa yetu 1,273 hapa Dodoma kwa hakika Mungu atasikia maombi yetu na mkoa wetu utakuwa na Amani"amesema Dkt Chilongani
Aidha ametoa shukrani kwa viongozi wote wa Kanisa la Anglikana DCT kwa kuendelea kusimama katika nafasi ya mwanga wa kiimani na kijamii, na kuwataka kutekeleza maagizo hayo kwa umoja na ari ya kuilinda nchi dhidi ya misukosuko.
Mwisho







0 Comments