Wautaka ujumbe wa Tanzania CoP30 kubeba agenda ya kuikoa bahari
NA. Mwandishi wetu
Wakati viongozi wa dunia na wataalamu wa mazingira wakijiandaa kukutana katika mkutano wa kimataifa wa kujadili hatua za kukabiliana na mabadiliko tabianchi (CoP30), unaotarajiwa kuanza Novemba 10 na kuhitimika Novemba 21,2025, uchafuzi wa bahari unaosababishwa na kuzagaa kwa taka ngumu ufukweni unawasababisha wakazi wa Pwani ya Dar es Salaam kulia kimya kimya.
Wingi wa taka ngumu hasa za plastiki unasababisha maeneo ya Kigamboni, Mbwamaji na Tungi jijini Dar es Salaam, kukumbwa na athari za moja kwa moja za mabadiliko tabianchi zinazosababishwa na uharibifu wa mazingira ya bahari kutokana na utupaji holela wa taka ngumu hasa chupa za plastiki ambazo huathiri mfumo wa ikolojia wa bahari na kuharibu makazi ya viumbe Bahari.
Mikoko inakauka, matumbawe yanaathirika na samaki wanapotea, hii inasababisha bei ya kitoweo hicho kupaa,cha kusikitisha zaidi hawana uelewa wowote wa namna ya kupambana na hali hiyo ingawa wanatamani kuwa mstari wa mbele kuikoa bahari ambayo wengi wao ni eneo lao la kujipatia kipato.
Ni jambo la kusikitisha, lakini upo uwezekano wa mkutano huo wa CoP30 ukaleta suluhisho la changamoto hiyo ingawa wananchi wengi waliozungumza na mwandishi wa Makala haya hawajui chochote kuhusu mkutano huo na umuhimu wake kwa nchi na wananchi.
COP30 ni jukwaa rasmi la kimataifa kwa ajili ya kujadili na kuamua malengo ya kukataa uzalishaji wa hewa ukaa, kutafuta ufadhili wa fedha za kukabiliana na madhara ya mabadiliko tabianchi na kufikia makubaliano ya kimataifa na sera za kitaifa za utekelezaji wake kama vile mkataba wa Kyoto na Paris.
Mkutano huu ni mwendelezo wa mikutano inayofanyika kila mwaka tangu mwaka 1995 ni moja ya majukwaa muhimu ya dunia kwa ajili ya kuweka mikakati na hatua za pamoja za kukabiliana na mabadiliko tabianchi.
Kutokana na ukubwa wa changamoto ya taka za plastiki kuzagaa kwenye fukwe za bahari, bila shaka ujumbe wa Tanzania utakaoshiriki mkutano wa CoP30 unaweza kuleta suluhisho la kudumu la tatizo hilo, kwa jiji la Dar es Salaam nag maeneo mengine ya nchi.
Ripoti za tathmini za uchafuzi wa plastiki zinaonyesha kuwa Jiji la Dar es Salaam linachangia kiwango kikubwa cha chupa za plastiki zote zinazoishia kwenye maji hapa nchini ikiwemo bahari, mito na maziwa.
Ripoti ya Mwongozo wa Kitaifa wa Kutambua Maeneo Hatari ya Plastiki na Kuunda Mikakati iliyooandaliwa na International Union for Conservation of Nature (IUCN) kwa kushirikiana na Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Mazingira (UNEP) na taasisi ya Life Cycle Initiative (chini mradi wa MARPLASTICCs), inabainisha kuwa, Jiji la Dar es Salaam linachangia asilimia 71 ya taka zote za plastiki zinazoishia baharini, mito na maziwa.
Kulingana na ripoti hizo za mwaka 2018 wastani wa tani 29,000 ziliingia kwenye maji (bahari, mito na maziwa) hapa nchini. Uchafuzi huu unatajwa kuzidisha athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo ya Pwani, huku umasikini wa wavuvi na wafanyabiashara wa samaki ukiongezeka.
Baadhi ya wakazi wa maeneo ya Mbwamaji na Tungi katika wilaya ya Kigambonim jijini Dar es Salaam, wanakiri kuwa hali ya mazingira ya Bahari kwa sasa si nzuri hasa katika maeneo ya ufukwe ambapo chupa za plastiki zimezagaa kwa kiwango kikubwa.
Juma Hassan, mfanyakazi wa Hoteli ya Mbongwe iliyopo Kigamboni Dar es Salaam, anaeleza kuwa, wanakusanya kiasi kikubwa cha chupa za plastiki kwa siku kutoka ufukweni ili kuyafanya mazingira yaendelee kuvutia kwa wageni.
"Siwezi kusema kiwango halisi cha ujazo wa chupa za plastiki tunazokusanya kwa siku kwa kuwa hatupimi, lakini ni nyingi," alisema.
Yohana Rwehemeja, mkazi wa Tungi anasema, mazingira ya bahari kwa sasa si mazuri hasa katika maeneo ya ufukwe kutokana na chupa za plastiki kuzagaa kwa kiwango kikubwa.
Chupa za plastiki ni tatizo kubwa, zimezagaa sana kwenye eneo kubwa la fukwe ya Kigamboni. Mbaya zaidi, chupa nyingi zinazoonekana ni zile ambazo hazifai kurejeleshwa, mara nyingi za vinywaji vya kuongeza nguvu, zinadumu kwa muda mrefu na kwa kiasi kikubwa zinaingia baharini na kuathiri viumbe vya baharini na mazingira ya ndani na nje ya bahari,"alisema Rwehemeja.
Mariam Kaulime, mfanyabiashara wa Samaki, Kigamboni, anasema biashara yake inazidi kuwa mbaya, akilinganisha hali ilivyokuwa miaka 10 iliyopita na sasa, ambapo bei ya samaki imepanda kwa kwa kuwa upatikanaji wake kuwa mgumu
Miaka 10 nyuma upatikanaji wa samaki ulikuwa wa kiwango cha juu. Kwa sasa, ndoo moja ya lita 20 iliyojaa samaki wadogo inaweza kununuliwa kwa Shilingi 75,000 hadi 90,000, wakati zamani tulikuwa tukiinunua kwa Shilingi 30,000 hadi 50,000," alisema Kaulime.
Hali hiyo inatokana na uchafuzi wa mazingira ya bahari ambapo makazi ya samaki yamevurugwa sababu ya uwepo wa taka ngumu na uvuvi haramu, hivyo wavuvi wanalazimika kwenda mbali zaidi.
Hata hivyo, wananchi wote hao walipoulizwa kuhusu suala la mabadiliko tabianchi walieleza kutojua chochote, lakinia pia hawajui kama utupaji wa chupa za plastiki baharini nao unachangia hali hiyo.
Kwa upande wake Hamdani Maluko na Mboka Ngereza ambao ni wakazi wa eneo la Mbwamaji kwa zaidi ya miaka 30 wanaeleza kuwa kabla ya mwandishi kuwaeleza masuala ya mkutano wa CoP30, hawakuwa wakijua chochote kuhusu mkutano huo.
Baada ya kupata uelewa wa awali juu ya mkutano huo, walitoa mapendekezo yao kwa serikali na wadau wa mazingira kuhakikisha wanaibeba agenda ya uchafuzi wa bahari unaosababishwa na taka za plastiki.
Akizungumzia umuhimu wa CoP30 kwa uhai wa bahari, Mhadhiri na mtafiti wa masuala ya Mabadiliko ya tabianchi kutoka Chuo Kikuu cha SAUT, Dkt. Aidan Msafiri, amesema kuna haja kwa ujumbe wa Tanzania unaokwenda COP30 kuibeba agenda ya uchafuzi wa bahari hasa utupaji wa chupa za plastiki baharini.
"Ujumbe wetu unaokwenda COP30 unapaswa kulichukua suala hili kama ajenda ya dharura na watumie vikao vya pembeni (side events) kuhakikisha wanaieleza dunia juu ya hatari hii inayotukabili," alisisitiza Dkt. Msafiri.






0 Comments